Habari,
na karibu tena katika muendelezo wa mafunzo yetu ya kilimo cha kisasa. Leo
tutaangazia kwenye mahitaji ya Udongo na Mbolea katika kilimo cha Mahindi.
Karibu …
Mahitaji ya udongo na mbolea ni muhimu kwa ajili ya ukuaji wa mmea wowote ule, hata hivo mahitaji hayo hutofautiana kati ya mmea moja na lingine kutokana na kutofautiana kwa sehemu ya zao (product) katika hiyo mimea (yaani economic part of a plant). Kwa mfano: mahindi, mpunga sehemu ya zao ni mbegu/punje, wakati nyanya, na bilinganya zao lake ni tunda nakadhalika viazi zao lake ni mizizi!
Hivyo basi mahitaji ya udongo na mbolea katika kilimo cha mahindi ni tofauti na mazao mengine, endelea....
UDONGO
Udongo una rutuba ya asili yaani virutubisho
katika udongo, mboji (organic
matter), na
viumbe mbalimbali vinavyoishi kwenye udongo. Rutuba ya udongo inategemea sana
hali ya udongo kikemia, kibiolojia na kifizikia.
Makundi Ya
Udongo
Kuna makundi makuu matatu ya udongo, kutokana na
ukubwa wa chengachenga
za udongo:
• Kichanga (Sand
soil) - una uwezo mdogo wa kuhifadhi maji
na unyevunyevu. Hivyo, hukauka upesi.
• Tifutifu (Loam
soil) - unahifadhi maji vizuri na
upatikanaji wa maji na virutubisho kwa mimea ni mkubwa.
• Mfinyanzi (Clay
soil) - unahifahdi maji mengi zaidi,
bali upatikanaji wa maji na virutubisho kwa mimea ni mdogo.
Vipimo vinavyoonyesha hali ya rotuba ya udongo ni:
• Tindikali ya udongo
• Kiasi cha mboji
• Kiasi cha Naitrojeni, Fosfati,
Potashi, Salfa, Chokaa (Calcium)
na Magnesium. Vilevile kiasi cha zinki, shaba, manganese na boroni vinapimwa.
pH ya udongo (Soil pH)
pH ni kipimo kinachoonyesha kiwango cha tindikali
au nyongo katika udongo. Udongo waweza kuwa tindikali (ph ndogo kuliko 7),
nyongo (ph kubwa kuliko 7), au katikati (neutral) - ph ya 7. Tindikali au nyongo ya udongo hupimwa kwa
kutumia pH mita. Mazao mengi hustawi zaidi katika udongo wenye hali ya
tindikali ya wastani (kipimo cha pH 5.5 hadi 7.0).
Mahindi hustawi kwenye udongo wa tifutifu wenye
tindikali ya wastani na virutubisho vya kutosha.
MBOLEA
Mbolea ni chakula cha mimea,
ambayo ni mchanganyiko wa virutubisho mbalimbali vinavyoongezwa kwenye udongo
au vinavyowekwa moja kwa moja kwenye mimea ili kuongeza ukuaji na uzalishaji wa
mimea.
Virutubisho hivyo ni pamoja
na madini muhimu kama vile naitrojeni, fosfati na potashi. Madini mengine ni
pamoja na salfa, chokaa (calcium), magnesium, boroni, shaba, chuma, manganese, molybedenum na zinki. Haya madini kwa
asili, yanapatikana katika udongo kwa viwango tofauti. Yanapopungua kutokana na
kilimo, inabidi yaongezwe kwa kutia mbolea.
Aina za mbolea
Kuna aina mbili kuu za
mbolea ambazo ni:
1. Mbolea za asili (organic fertilizers)
2. Mbolea za viwandani (inorganic
or industrial fertilizers)
Mbolea Za Asili (Organic Fertilizers)
Hizi ni mbolea zinazotokana
na wanyama na mimea. Mbolea za asili ni kama vile:
i. Mbolea vunde: inajulikana
pia kama biwi au compost. Hutokana na mchanganyiko wa manyasi au mabaki ya mbao na samadi na
majivu.
ii. Samadi: kutoka
kinyesi cha wanyama kama mifugo na ndege.
iii. Mbolea za kijani: hutokana
na kupanda mimea aina ya mikunde ambayo hukatuliwa na kuchanganywa na udongo.
iv. Majivu: ni mbolea ya
asili yenye madini aina ya potashi kwa wingi, fosfati, chokaa na magnesium.
v. Matandazo (mulch):
ambayo baadaye yakioza huwa mbolea.
Mbolea
Za Viwandani (Inorganic Fertilizers)
Hizi ni mbolea
zinazotengenezwa viwandani kwa kutumia virutubisho mbalimbali kwa kufuata
viwango maalum vilivyowekwa ili kukidhi mahitaji ya mimea. Mbolea hizi
zinatengenezwa kwa lengo maalum la kupata aina na kiasi fulani cha kirutubisho/
virutubisho vinavyohitajika na mimea.
Mbolea Za Kupandia Mahindi
Mbolea maarufu za kupandia
katika soko la Tanzania ni: TSP, DAP, Minjingu Phosphate na Minjingu Mazao.
Lakini zile ambazo zimechaguliwa kwenye mradi wa ‘Kukuza matumizi ya Minjingu Phosphate’
ni DAP, Minjingu Phosphate
na Minjingu Mazao.
1.
Diammonium Phosphate (DAP)
Ina virutubisho viwili - naitrojeni
ambacho kiko kwa kiwango cha asilimia 18, na fosfati (P2O5) ambacho kiko kwa
kiwango cha asilimia 46. Inapatikana katika hali ya chengachenga (granules).
2. Minjingu Phosphate
Ina kiwango cha fosfati
(P2O5) asilimia 29 na inatumika zaidi kwa kutoa kirutubisho hiki. Lakini
inaongeza vilevile kirutubisho cha chokaa (calcium) ambacho kipo kwa kiwango cha
asilimia 40. Chokaa inasaidia vilevile kukabili tindikali (acidity)
ya udongo.
3. Minjingu Mazao
Hii ni mbolea mpya
inayotokana na Minjingu Phosphate lakini imeongezwa virutubisho vingine vitano
ambavyo ni naitrojeni (10%), salfa (5%), zinki (0.5%), shaba (0.5%), boroni
(0.1%), pamoja na chokaa (25% CaO) na magnesium (1.5% MgO). Virutubisho
vilivyoongezwa hususani naitrojeni na salfa ni vile ambavyo vinakosekana katika
aina nyingi za udongo.
Zinki, shaba na boroni
vimeongezwa kwa tahadhari kwa sababu vinaonyesha dalili za upungufu katika
baadhi ya maeneo. Minjingu Mazao iko katika hali ya chengachenga.
Jinsi
ya kuchagua mbolea ya kupandia
Mbolea za kupandia hasa
Minjingu Phosphate na Minjingu Mazao zinahitaji hali maalum ya udongo ili
ziweze kufanya kazi vizuri.
Kwa mfano hali ya tindikali
ya udongo inabidi iwe chini ya 6.2 ili mbolea za Minjingu ziyeyuke kwa kiwango
cha kutosha. Kwa udongo wenye tindikali zaidi ya 6.2, tumia DAP wakati wa
kupanda. Ikiwa kuna upungufu wa potashi, tumia mbolea zinazorejesha madini
hayo.
Tumia mboji pamoja na mbolea
za viwandani ili kuongeza mazao. Mboji huwa haibebwi na mvua na faida yake
hudumu kwa muda mrefu. Mboji husaidia udongo kuhifadhi maji na virutubisho.
Zinapowekwa kwenye mashimo ya kupandia mbegu ni vyema kufukia mbolea kabla ya
kuweka mbegu (kutenganisha mbolea na mbegu).
Dalili Ya Upungufu Wa
Virutubisho Mbalimbali
1. Upungufu Wa Naitrojeni (Nitrogen)
Kwa ujumla mmea unakuwa
mdogo, mwembamba na hutoa suke dogo, na mwishowe hutoa mazao kidogo (picha
A). Kama upungufu ni mkubwa
sana mmea unaweza usitoe mhindi kabisa.
Kupungua kwa kasi ya ukuaji
wa mmea - ambayo husababisha mmea kudumaa. Rangi ya kijani kwenye mmea hufifia
na kugeuka taratibu kuelekea kwenye njano. Upungufu ukiwa mkubwa sana, majani
hugeuka rangi ya njano kutoka pembeni. Majani yaliyokomaa ndio huanza kugeuka.
Majani ya mwanzo hukauka mapema kwenye mimea yenye upungufu kuliko ile yenye
naitrojeni ya kutosha.
2. Upungufu Wa Fosfati (Phosphorus)
Dalili ya kwanza ni kupungua
kwa kasi ya kukua na mashina kuwa membamba.
Upungufu ukiwa mkubwa, mmea
unakuwa na rangi ya zambarau. Rangi hii inaanzia pembeni
mwa majani na kwenye mashina na baadaye husambaa kwenye jani lote. Rangi
inaonekana vizuri zaidi upande wa chini wa jani. Majani ya mwanzo hukauka
mapema na mizizi haikui vizuri kwenye mimea yenye upungufu kuliko ile yenye
fosfati ya kutosha.
3. Upungufu Wa Potashi (Potassium)
Kupungua kasi ya ukuaji wa
mimea, ambayo inasababisha mmea kudumaa.
Upungufu ukiwa mkubwa rangi
ya kijani inafifia na mwisho kutoweka kabisa na sehemu iliyoathirika inakauka (necrosis)
kwenye mazao mengi kama
mahindi, mazao mengine ya nafaka na miti ya matunda. Kutoweka kwa rangi ya
kijani na kukauka kunaanzia pembeni mwa majani na kwenye ncha. Majani yanakuwa
na michirizi ya manjano na vinundu nundu kama migongo ya bati (yellowish
streaks and corrugated).
Majani ya mwanzo hukauka mapema kwenye mimea yenye upungufu kuliko ile yenye
potashi ya kutosha.
Manufaa ya matumizi ya mbolea
i). Kuongeza mavuno
ii). Ubora wa mazao
iii). Kuhifadhi rutuba ya
udongo
iv). Kuongeza kipato
kutokana na mavuno mengi na bora
Mambo muhimu ya kuzingatia
Ni muhimu kutumia mbolea za
viwandani katika kilimo cha mahindi ili kumuwezesha mkulima kupata mavuno
mengi. Lakini ikumbukwe kwamba matumizi ya mbolea ni lazima yaambatane na
matumizi ya mbinu nyingine bora za kuzalisha mahindi, kama vile:
·
Kuandaa
shamba
·
Matumizi
ya mbegu bora
·
Kupalilia
·
Kupiga
madawa ya kuzuia na kuua wadudu na magonjwa
·
Kuvuna
kwa wakati unaostahili
·
Kuhifadhi
vizuri mahindi
kwa kumalizia:
Mahitaji
ya udongo na mbolea ni muhimu kwa ajili ya ukuaji wa mmea wowote ule,
hata hivo mahitaji hayo hutofautiana kati ya mmea moja na lingine
kutokana na kutofautiana kwa sehemu ya zao (product) katika hiyo mimea
(yaani economic part of a plant). Kwa mfano: mahindi, mpunga sehemu ya
zao ni mbegu/punje, wakati nyanya, na bilinganya zao lake ni tunda
nakadhalika viazi zao lake ni mizizi!
Hivyo basi ni muhimu ujue zao unalotaka kulima linahitaji nini katika udongo na mbolea ili ufanye maamuzi sashihi.
Acha comment yako hapa chini kwa mchango wowote ule. Pia waweza kuwasiliana nasi
Labels: KILIMO BORA, KILIMO CHA MAHINDI