Zao
hili hustawi maeneo mengi Nchini Tanzania. Viazi hustawi vizuri katika maeneo
ya tambarare yenye udongo tifutifu, unaoruhusu maji kupenya kwa urahisi. Udongo
wa mfinyazi na wenye kokoto nyingi haufai kwani huzuia mizizi kupenya na
kupanuka.
Utangulizi
Kilimo
cha Viazi Vitamu ni muhimu sana kwani viazi vitamu ni moja kati ya
mazao makuu ya mizizi katika jamii ya ki-Tanzania. Zao hili ni moja kati ya
mazao ya kinga ya njaa kutokana na sifa yake ya kuvumilia ukame. Viazi vitamu
asilia yake ni Amerika ya Kati na ya Kusini. Nchini Tanzania, zao hili hulimwa
zaidi katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Dodoma, Morogoro, Kagera, Arusha na
Ruvuma.
Matumizi
Viazi vitamu hutumika kama
chakula kwa kutayarishwa katika njia mbalimbali kama vichembe, na Matobolwa.
Pia Unga wa viazi vitamu hutumika kutengeneza vyakula kama keki, maandazi,
kalimati, tambi na Juice. Majani ya viazi huliwa kama mboga (matembele) pia
hutumika katika kutayarisha mboji.
Aina
Kuna aina nyingi za viazi
vitamu zinazolimwa ulimwenguni. Hapa nchini Tanzania aina zinazolimwa zaidi ni
Ukerewe, Simama, Kakamega, Karoti C, Mwananjemu, Ali mtumwa mayai, Mavuno,
Pananzala, Kibakuli, Sinia, Vumilia na Polista.
Uzalishaji
Zao hili hustawi maeneo mengi
Nchini Tanzania. Kilimo cha Viazi
Vitamu kinakubali vizuri zaidi katika maeneo ya tambarare yenye udongo
tifutifu, unaoruhusu maji kupenya kwa urahisi. Udongo wa mfinyazi na wenye
kokoto nyingi haufai kwani huzuia mizizi kupenya na kupanuka. Shamba jipya
litayarishwe vizuri kwa kufyeka vichaka na kung’oa visiki. Majani yafukiwe
wakati wa kutengeneza matuta ili kuongeza rutuba ya udongo.
Viazi vipandwe kwa kutumia marando
(mashina ya viazi) yenye urefu wa sentimita 30 kwa mavuno bora. Inashauriwa kutumia
sehemu ya juu ya shina kwa mavuno zaidi. Marando yapandwe katika umbali wa
sentimita 25 hadi 30 kutoka mmea hadi mmea na sentimita 60 hadi 75 kutoka tuta
hadi tuta. Viazi pia vyaweza kupandwa kwa kutumia viazi vyenye afya vyenye
uzito wa kati ya gramu 20 hadi 30. Hata hivyo inashauriwa kutumia marando ili
kupata mavuno zaidi na kuepuka kuenea kwa magonjwa.
Kutunza shamba
Ni muhimu kupalilia shamba
katika miezi miwili ya mwanzo ili kuupa mmea nguvu ya kutambaa vizuri. Baada ya
muda huo, viazi huweza kufunika ardhi na hivyo huzuia uotaji wa magugu. Mashambulizi
ya wadudu kama vile kipepeo, mbawa kavu, fukusi na minyoo fundo ni miongoni mwa
changamoto zinazokikabili kilimo cha viazi vitamu. Pia hushambuliwa na magonjwa
yakiwemo magonjwa yanayotokana na virusi kama Sweet Potato Chlorotic Stunt
virus (SPCSV). Magonjwa na wadudu yaweza kudhibitiwa kwa kuzingatia usafi
wa shamba, kubadilisha mazao, na kuzingatia udhibiti sango.
Uvunaji
Uzuri wa kilimo cha Viazi
vitamu ni kwamba huchukua mda mfupi sana kukomaa, hivyo kumlipa mkulima mapema
kabisa. Kwa kawaida huwa tayari kuvunwa miezi mitatu hadi minne tangu kupandwa
kutegemeana na hali ya hewa. Viazi vinaweza kuvunwa kidogo kidogo kwa kutumia
mikono, vijiti, jembe, au rato kadri vinavyohitajika. Aidha inashauriwa viazi
visiachwe ardhini muda mrefu bila kuvunwa kwani vitakomaa sana na kuwa na
nyuzi, na hivyo kuharibu ubora wake. Pia kuacha viazi muda mrefu hukaribisha
mashambulizi ya wadudu kama fukusi na kuoza. Kwa maeneo makubwa zaidi,
inashauriwa kutumia mashine ya kukokotwa na ng’ombe. Uvunaji ufanywe kwa
uangalifu ili kuhakikisha viazi visikatwekatwe wala kuchubuliwa wakati wa
kuvuna.
Mavuno ya viazi hutofautiana kulingana na aina, hali ya hewa, na udongo. Mavuno ya viazi yanakadiriwa
kufikia tani 20 kwa hekta.
Labels: KILIMO BORA, VIAZI VITAMU