Wadudu waharibifu wa nyanya na dawa zake

Ili uweze kubaini mapema uwepo wa wadudu waharibifu au magonjwa katika mimiea yako ya nyanya ni lazima uwe unachunguza mimea yako mara kwa mara. Angalia uwepo wa wadudu kwenye sehemu ya chini ya majani, juu yake, kwenye mashina, maua au matunda kama yametobolewa au la.


Sasa ungana nami katika makala hii uweze kujua ni wadudu wepi waharibifu kwenye zao lako la nyanya shambani kwako ili uweze kukabiliana nao. Pia waweza kujua magonjwa ya nyanya na dawa zake hapa


1. Funza wa vitumba: American bollworm (Helicoverpa armigera)

Kubaini mapema mayai au funza kabla hayajatoboa matunda ni muhimu sana. Funza wachanga kwanza hula majani baadae matunda. Funza wakishaingia ndani ya matunda husababisha uharibifu mkubwa. Uharibifu kwenye matunda machanga husababisha kupukutika kwake, wakati mashambulizi ya matunda yaliyokomaa husababisha matundu ambayo huruhusu kuingia kwa aina nyingine za ukungu na bakteria ambao huleta madhara zaidi.

funza-wa-vitumba-anavyotoboa-matunda-ya-nyanya
Funza wa vitumba anavyotoboa nyanya


Kipepeo chake huwa na rangi ya manjano-kahawia chenye doti iliyokoza, mistari isiyo sawa ya kijivujivu na alama nyeusi yenye umbile la figo kwenye mbawa za mbele. Mbawa za nyuma ni nyeupe na baka jeusi katika sehemu za nje. Kipepeo huwa na urefu wa 14-18mm na upana wa mbawa wa 35-40mm.

Namna ya kudhibiti

Kubainika mapema hupatikana kwa kuchunguza mazao kila mara. Angalia majani yaliyo chini ya maua ya juu yaliyochanua kwa kutafuta mayai ya viwavi tumba/dukari. Baada ya kubainika kwa funza huyu fuata mbinu zifuatazo:

Mbinu bora za kilimo

•Chuma na teketeza matunda yaliyoathirika.
•Ondoa na teketeza mabaki ya mazao baada ya kuvuna.
•Chimbulia ardhi baada ya mavuno.
•Fanya mzunguko wa mazao.
•Toa kwa mkono na teketeza mayai na funza wadogo wadogo.
•Epuka kupanda nyanya karibu na pamba au mahindi.
•Changanya mazao, panda na pilipili na maua bange (African marigold).

Dawa (Chemical control)

Mara nyingi dawa (kemikali) inayodumu kwa muda mfupi ndio inayohitajika kwani matunda hushambuliwa muda mfupi kabla ya kuvuna. Kwa hivyo, dawa kama vile mevinphos na endosulfan zinashauriwa kutumika. Dawa nyingine zilizosajiliwa kutumika kwa mdudu huyu ni carbaryl, tetrachlorvinphos, methomyl, acephate, monocrotophos na dawa zenye pareto.

Kibaiolojia (Biological control)

Funza wa vitumba wana maadui wengi asilia wakiwemo viumbe wanaokula mayai (kama Trichogramma spp.), wanaoshambulia funza (nyigu na nzi wanaokula funza) na washambulizi kama vile aina za maji moto, assassin bugs, minute pirate (anthocorid) bugs, lacewings na ladybird beetles. Kuku na ndege pia hula mafunza na mabuu wakati fulani katika ukuaji wa matunda. Madawa ya kibaiolojia hujumuisha Muarobaini (Azadirachta indica) na Bt (Bacillus thuringiensis). Madawa yatokanayo na Bt yanayouzwa kwa udhibiti wa mafunza hujumuisha Dipel, Thuricide (zote ni aina za Bt kurstaki), Florbac 70 DG na XenTari (zote ni aina za Bt aizawai).

Yafahamu magonjwa hatari ya nyanya na jinsi ya kukabiliana nayo

2. Utitiri Mwekundu: Red spider mites  (Tetranychus urticae)

Utitiri wekundu huwa ni tatizo hasa wakati wa kiangazi. Utitiri huu unaweza kutambulika kwa kutumia lenzi ya mkono. Dalili za awali hujumuisha madoa ya manjano, ambayo hujitokeza pale mashambulizi yanapokuwa makubwa; baada ya hapo njano kubwa na ishara za kama kuungua hujitokeza kwenye majani na matunda ikifuatiwa na utando kama wa buibui.

Utitiri-mwekundu-wa-nyanya-ulivyotanda-kwenye-jani-la-nyanya
Utitiri mwekundu


Mashambulizi makubwa husababisha umanjano wa majani na matunda, kupukutika mapema kwa majani, kukauka kwa mti kuanzia kileleni na kufa kwa mmea. Vichungu vya utitiri wekundu hujikusanya kwenye ncha za majani wakati idadi ya utitiri wekundu inapozidi chakula kilichopo.

Namna ya kudhibiti

Fanya uangalifu wa kubaini utitiri wekundu kwenye mazao na chukua hatua mara unapowabaini. Matumizi ya dawa muafaka haraka pale tu utitiri wekundu wanapobainika, husaidia kupunguza athari.

Mbinu bora za kilimo

•Weka matandazo na mwagilia
•Ngo’a na choma moto mimea iliyoathirika
•Choma moto mabaki yote ya mazao baada ya kuvuna
•Fanya mchanganyiko wa mazao na vitunguu maji au vitunguu swaumu

Dawa (Chemical control)

Tumia dawa za kemikali pale tu utakapowabaini, na baada ya hapo tumia dawa za aina mbali mbali kwa kupishana kuzuia usugu wa utitiri wekundu. Aina nyingi za madawa zinaweza kutumika, kama vile Dimethoate, Abamectin, Bifenthrin na acephate.

Kibaiolojia (Biological control)

Aina ya utitiri shambulizi ni adui asilia wa utitiri wekundu anayepatikana kwenye maduka yanayouza viumbe washambulizi kwa matumizi kwenye jengo la kuoteshea mimea na hufanya kazi vizuri wanapodhibitiwa vyema. Hii inahitaji udhibiti mzuri bila ya kutumia madawa ya kemikali ya kuulia wadudu. Matumizi ya dawa za kemikali za kuulia wadudu zinaweza zikasababisha kutofanya kazi vizuri kwa viumbe hawa kwani wadudu wanaokula chawa wekundu huuliwa na dawa hizi.

3. Minyoo Fundo: Root knot nematodes (Meloidogyne spp.)

Dalili za minyoo fundo hujumuisha kupiga umanjano na kudumaa kwa mimea na hatimaye kunyauka wakati wa jua kali. Mimea iliyoathirika hujitokeza shambani kwa sehemu sehemu. Mashambulizi husababisha kupungua kwa mazao ikitegemea ukubwa wa mashambulizi kwenye mizizi, mashambulizi makubwa husababisha kufa kwa mimea. Mimea huwa na stahimili ndogo kwa magonjwa mengine.

Minyoo-fundo-kwenye-mizizi-ya-nyanya
Minyoo fundo


Mimea inapong’olewa kutoka kwenye udongo, mizizi huonekana imevimba yenye maumbile mabaya na vifundo, yanayojulikana kama mafundo ya mizizi. Ukubwa wa vifundo hivi unaweza kuwa sawa na ukubwa wa kichwa cha pini ya kirungu mpaka 25mm au zaidi. Mashambulizi makubwa husababisha mzizi wote ukawa na umbile baya na mafundo ambao hatimaye huoza. Mashambulizi yanayofuata husababisha uharibifu na dalili za magonjwa huongezeka kwenye nyanya.

Namna ya kudhibiti

Mimea mingi inayopandwa huwa na minyoo fundo. Minyoo huweza kuingizwa shambani kupitia miche kutoka vitaluni au kwa usambaaji kutoka shamba hadi shamba katika maeneo yenye mashambulizi. Hatua zifuatazo zinaweza kuchukuliwa ili kudhibiti minyoo ya mimea.

Mbinu bora za kilimo

•Tumia mimea ya mitego kama vile Mbange ‘marigold’ (Tagetes spp.) na haradali ya India.
•Dumisha kiwango kikubwa cha mbolea za asili (samadi na mboji) katika udongo.
•Changanya mashudu (mabaki) ya muarobaini na udongo.
•Tumia aina zenye kustahimili minyoo fundo (kama Caracas, Kentom, Meru, Piersol, Roma VFN, Tengeru 97, Zest F1, Star 9001 na Star 9003).
•Zungusha mazao na vitunguu maji, mahindi madogo, mahindi matamu, mahindi, mtama, uwele, ufuta, au nyasi. Mbinu ya mzunguko wa mazao unaojulikana kama “STRong” unashauriwa kutumika katika udhibiti wa minyoo fundo. Mbinu hii inashauri kupandwa kwa mmea usiostahimili (kama Nyanya), ikifuatiwa na zao lenye kustahimili kidogo (kama Kebeji), halafu zao lenye kustahimili kabisa (kama Vitunguu maji), kabla ya kurejea tena zao lisilostahimili (kama Nyanya).
•Ng’oa mizizi na uchome moto mimea iliyoathirika na takataka zote za mazao.
•Ua vimelea vya maradhi kwenye vitalu kwa kutumia moto au mvuke kabla ya kusia mbegu.
•Epuka kupandikiza miche iliyoathirika.
•Tumia mbinu za kibaiolojia kwa kutumia bidhaa zinazotokana na Trichoderma.

Dawa (Chemical control)

Minyoo fundo inaweza kudhibitiwa kwa kutumia dawa ya minyoo/wadudu (Vydate L) na dawa za kufukiza (Telone II, Telone C-17, Vapam), lakini hizi hazipatikani kwa urahisi.

Kibaiolojia (Biological control)

Udhibiti wa kibaiolojia unahusisha matumizi ya viumbe wapinzani wa minyoo fundo (kama ukungu na bacteria). Kuna aina nyingi za ukungu zinazokula minyoo. Baadhi ya aina za ukungu (Arthrobotryts spp. na Monacrosporium spp.) hutumia nyuzi zao na mbegu zinazoganda kama mitego ya kunasia minyoo, aina nyingine za ukungu (kama Pochonia chlamydosporia, Trichoderma spp. na Paecilomyces lilacinus) hufyonza mayai na minyoo jike. Aina za bakteria maarufu wapinzani wa minyoo ni Pasteuria penetrans na Bacillus spp.

4. Sota (Cutworms)

Hushambulia miche ya nyanya hasa baada ya kupandikizwa shambani. Wakati wa mchana hujificha kwenye udongo na usiku hujitokeza na kukata miche kwenye shina usawa wa udongo.

Sota: wadudu waharibifu wa mimea ya nyanya


Namna ya kudhibiti

· Nyunyiza dawa za kuua wadudu (kama Rogor, Actellic, Selecron, Dursban) kwenye shina usawa wa udongo
· Hakikisha miche inapata maji ya kutosha

Yafahamu magonjwa hatari ya nyanya na jinsi ya kukabiliana nayo 

5. Vidukari au Wadudu mafuta (Aphids)

Ni wadudu wenye rangi nyeusi au kuijani au kahawia. Hukaa chini ya majani na kufyonza utomvu kwenye majani machanga. Hudumaza mmea na kushindwa kuzaa matunda

Aphids-wa-nyanya
Wadudu mafuta

Namna ya kudhibiti

Nyunyizia dawa za sumu za kuulia wadudu kama Rogor, Actellic, Selecron, Dursban maji ya majani ya mwarobaini na utupa, maji ya pilipili.

6. Inzi weupe (White flies)

Hawa ni Inzi weupe wadogo sana. Hujitokeza sana wakati wa kiangazi. Wadudu hawa hueneza ugonjwa wa nyanya wa virusi ujulikanao kama Rasta.

Whiteflies-kwenye-jani-la-nyanya
Nzi weupe kwenye jani la nyanya

Namna ya kudhibiti


Nyunyizia dawa za sumu za kuulia wadudu kama Selecron, Actellic, Dursban na thionex. Pia maji ya majani ya mwarobaini na utupa.

Haya sasa ni zamu yako, tuambie ni nini ulifanya ulipokumbana na wadudu kwenye shamba/bustani yako ya nyanya? je ulitumia dawa gani ambayo ungependa kumshauri mkulima mwenzako nae aitumie? Au bado wadudu wanaukusumbua shambani kwako? Acha comment yako hapa!

Labels: ,