UTANGULIZI
Jina la kitaalamu ni Zingiber officinale. Tangawizi ni aina ya zao la kiungo ambalo sehemu inayotumika ni tunguu (rhizome) ambalo huonekana kama mizizi ya mmea. Asili ya zao hili ni maeneo ya kitropiki ya bara
la Asia na hasa katika nchi za India na China. Zao hili linazalishwa kwa wingi
kutoka katika nchi ya Jamaica. Hapa nchini zao hili hulimwa katika mikoa ya
Kigoma, Tanga, Morogoro, Pwani, Mbeya na Kilimanjaro.
Tangawizi
hutumika kama kiungo katika kuongeza ladha, harufu na kuchangamsha katika
vinywaji (kama soda, juisi, vilevi n.k) na vyakula mbalimbali kama mikate,
biskuti, keki, nyama za kusaga, achari n.k. Hutumika pia katika viwanda
vinavyotengeneza madawa ya tiba mbalimbali kama dawa za meno, kikohozi, tumbo
na muwasho wa ngozi n.k. pia hutumika katika vipodozi kama poda n.k).
AINA
ZA TANGAWIZI
Hakuna
uthibitisho wa aina za tangawizi ambazo hulimwa hapa nchini ila kuna dalili ya
kuwa na aina za White Africa (Jamaica) na Cochin (flint); hii huwa na tunguu
ngumu zenye nyuzi.
TABIA
YA MMEA
Tangawizi
ni mmea unaotambaa chini ya ardhi, wakati wa masika hutoa majani juu ya ardhi.
Jamaica ina rangi hafifu ya kahawia na tunguu fupi wakati Cochin ina tunguu
fupi zaidi lenye ngozi ya rangi iliyo kati ya kijivu na nyekundu. Mmea una
urefu wa futi mbili na majani yake ni membamba marefu ambayo hufa kila mwaka
yakiacha tunguu ardhini likiwa hai. Maua ya mmea huu yana rangi nyeupe au
manjano.
|
Mmea wa tangawizi |
HALI
YA HEWA NA UDONGO
Zao
hili hustawi katika maeneo yenye hali ya kitropiki, kutoka usawa wa bahari hadi
mwinuko wa mita 1,500 au zaidi. Huhitaji mvua kiasi cha mm.1,200-1,800 na joto
la wastani wa nyuzi za sentigredi 20-25. Hustawi vema katika udongo tifutifu
wenye rutuba na usiotuamisha maji.
UPANDAJI
Zao
la tangawizi hupandwa kwa kutumia vipande vya tunguu vyenye kichipukizi kizuri
angalau kimoja na huweza kukatwa katika urefu wa sm.2.5-5. Wakati mwingine,
vichipukizi vinavyopatikana katika kumenya tangawizi huweza kuhifadhiwa na
kutumika kwa kupanda. Kiasi cha kilo 840-1700 cha vipande vya tunguu huweza
kutumika kwa kupanda katika hekta moja.
Nafasi
inayotumika kupanda ni kati ya sentimita.23-30 kwa 15-23 na kina cha
sentimita.5-10 na mara nyingi hupandwa katika matuta. Baadhi ya mazao huweza
kupandwa katika shamba la tangawizi ili kuweka kivuli chepesi ingawa si lazima
kivuli kiwepo. Inashauriwa kumwagilia maji endapo mvua inakosekana.
Soko la
tangawizi lipo ndani na nje ya nchi, kiasi kikubwa kinauzwa nchini. Bei yake ni
kati ya Tsh. 4000 - 6,500/- kwa kilo (Soko Kuu Morogoro. June, 2016). Bei hutofautiana
kulingangana na masoko, ulizia soko la karibu yako.