Kaya
nyingi hapa nchini hujihusisha na ufugaji wa kuku kwa lengo la kujipatia
chakula na kipato. Mazao yatokanayo na ufugaji wa kuku ni pamoja na mayai,
nyama, mbolea na manyoya kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Mifumo ya ufugaji
kuku ambayo hutumika hapa nchini ni huria, nusu huria na shadidi. Ufugaji wa
kuku utakuwa endelevu na wenye tija kwa kufuata kanuni za ufugaji bora
zifuatazo:-
• Kufuga kuku kwenye banda bora
• Kuchagua kuku bora wa kufuga
• Kutunza na kulisha kuku
kulingana na hatua mbalimbali za ukuaji
• Kudhibiti na kutibu magonjwa ya
kuku
• Kutunza kumbukumbu
BANDA LA KUKU
Kuku
huhitaji banda bora ili wasiathirike na madhara mbalimbali. Banda bora la kuku
linatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:-
• Imara, lenye uwezo wa
kuwahifadhi kiafya na pia dhidi ya hali ya hewa hatarishi kwa mfano jua kali,
upepo, baridi na mvua pamoja na wanyama hatari,
• Lenye mwanga,
hewa na nafasi ya kutosha inayoruhusu usafi kufanyika kwa urahisi,
• Lijengwe
sehemu yenye mwinuko isiyotuama maji, isiyo na upepo mkali na iwe mbali kidogo
na nyumba ya kuishi watu.
• Liwe na
vichanja kwa ajili ya kuku kupumzika na kulala
• Liwe na sehemu
ya kuwekea chakula, maji, kutagia, kuatamia na sehemu ya kulelea vifaranga
• Liwe na nafasi
ya kutosha kulingana na idadi ya kuku na kuweka vyombo vya chakula na maji
• Kwenye
mazingira ya joto banda liwe la ukuta mfupi na sehemu kubwa wazi yenye wavu hadi
kufikia kwenye paa
• Kwenye
mazingira ya baridi banda liwe na ukuta mrefu unaokaribia paa na sehemu ndogo
tu iwe wazi yenye wavu ili kupitisha hewa na mwanga
Vifaa vinavyotumika kwa ujenzi wa banda
Vifaa
vya kujengea banda vizingatie gharama na upatikanaji wake katika eneo husika.
Baadhi ya vifaa hivyo ni kama ifuatavyo:-
• Sakafu Saruji,
udongo, mbao, mianzi au fito
• Kuta Fito,
mabanzi, mbao, nguzo mianzi,udongo, matofali, mawe, mabati na wavu
• Paa Nyasi,
makuti, majani ya migomba, mabati na vigae.
• Wigo Matofali,
mbao, fito nguzo, mabanzi, mianzi, matete, wavu na mabati
Ukubwa wa banda
Ukubwa wa banda utategemea idadi ya kuku na aina ya kundi la
kuku. Kuku wanahitaji nafasi tofauti kutegemea umri, aina, na njia ya ufugaji.
Eneo la mita moja ya mraba linatosha kwa vifaranga 16 wa umri wa wiki 1 - 4.
Hivyo banda lenye mita za mraba 16 linaweza kulea vifaranga 320 hadi wiki 4.
Baada ya wiki 4 eneo hili liongezwe kutegemea aina ya kuku na njia inayotumika
katika ufugaji kama inavyoonekana kwenye Jedwali Na. 1
Jedwali Na 1: Eneo Linalohitajika Kufuga Kuku Kwenye Sakafu
ya Matandazo Kutegemea na Umri na Aina ya Kuku
Umri
wa kuku
|
Idadi
ya kuku kwa mita 1 ya mraba
|
Kuku
wa mayai
|
Kuku
wa nyama
|
Siku
1 hadi wiki 4
|
18
|
18
|
Wiki
ya 5 hadi ya 8
|
9
|
9
|
Wiki
ya 9 hadi 20
|
6
|
-
|
Wiki
21 na kuendelea
|
3 - 4
|
-
|
Angalizo:
Mabanda
yanayozungushiwa wigo kama ilivyo katika mfumo wa nusu huria, kuku mmoja
huhitaji eneo la wazi lenye ukubwa wa mita za mraba 10. Mfano, kuku 100
huhitaji eneo la mita za mraba 1000
Vifaa na Vyombo Muhimu
Mfugaji
anashauriwa kutumia vifaa na vyombo maalum ili kurahisisha na kuboresha
utunzaji wa makundi mbalimbali ya kuku. Vifaa na vyombo vinavyohitajika kwa ajili
ya kuwekea chakula na maji, kutagia mayai na kupumzikia vinapatikana kwenye
maduka ya pembejeo za mifugo. Aidha, mfugaji anaweza kutengeneza mwenyewe kwa
kutumia malighafi zilizopo kwenye mazingira yake.
KUCHAGUA KUKU BORA WA KUFUGA
Kuku wa Asili
Aina za
kuku wa asili wanaopatikana hapa nchini ni pamoja na Kuchi (Kuza), Poni
(Kishingo), Njachama, Kinyavu, Mbuni na Tongwe (Msumbiji). Mfugaji anaweza
kuongeza uzalishaji kwa kuchagua kuku mwenye sifa zifuatazo:-
• Uwezo wa kutaga mayai mengi
(kati ya 15-20) katika mzunguko mmoja wa utagaji (Jedwali Na 2),
• Uwezo wa kuatamia na kuangua
vifaranga wengi,
• Uwezo wa
kustahimili magonjwa,
• Anayetoka maeneo yasiyo na
magonjwa; na
• Umbo kubwa na kukua haraka.
Jedwali Na 2: Masuala ya
Kuzingatia Wakati wa Kumchagua Kuku Mtagaji wa Kienyeji
Viungo vya mwili
|
Sifa
|
Macho
|
Maangavu,
yenye wekundu kwa mbali na makubwa yamejaa kwenye soketi za macho.
|
Mdomo
|
Wenye
rangi ya njano kwa mbali
|
Kisunzu/upanga
|
Chekundu,
laini, kimelala kidogo upande na kinang’aa
|
Shingo
|
Iliyosimama
|
Umbali
kati ya kidari na nyonga
|
Upana wa
vidole 3-4 vya mpimaji
|
Upana wa
nyonga
|
Upana wa
vidole 3 vya mpimaji
|
Kuku wa Kisasa
Kuku bora
wa kisasa kwa ajili ya mayai au nyama ni mwenye sifa zifuatazo:-
• Uwezo wa kuanza kutaga wakiwa
na umri mdogo (miezi 5 - 6) kutegemea na koo,
• Umbo kubwa na anayekua haraka
(kilo 1.5-2.0 kwa kipindi cha wiki 8-12) kutegemea na koo kwa kuku wa nyama,
• Anayetaga mayai mengi (250 au
zaidi) kwa kuku wa mayai kwa mwaka; na
• Awe na uwezo wa kutaga katika
umri wa miezi 6 - 8.
Kuchagua Jogoo Bora wa Mbegu
Jogoo
wa mbegu anatakiwa awe na sifa zifuatazo:
• Achaguliwe kutoka kwenye koo
zenye sifa ya kutaga mayai mengi,
• Mrefu, umbo kubwa, miguu imara
na yenye nguvu,
• Awe machachari, ushawishi kwa
mitetea na ari ya kupanda; na
• Uwezo wa kupanda akiwa na umri
wa miezi 7 – 10.
|
Kuchi chotara |
Mayai kwa Ajili ya Kutotoa Vifaranga
Uchaguzi wa Mayai
Mayai
kwa ajili ya kutotoa vifaranga yawe na sifa zifuatazo:-
• Yaliyorutubishwa na jogoo,
• Yasiwe na nyufa,
• Yasiwe na maganda tepetepe,
• Yasiwe na kiini kilichovunjika,
• Yawe na ukubwa wa wastani; na
• Yasiwe yamekaa zaidi ya wiki 2
baada ya kutagwa.
Utunzaji wa Mayai
Mayai
ya kienyeji kwa ajili ya kutotoa vifaranga yatunzwe kwa kusimamishwa wima
sehemu iliyochongoka ikiwa imeangalia chini kwa siku 3 za mwanzo na kisha
yageuzwe ili sehemu iliyo butu iangalie chini. Mayai yahifadhiwe kwenye sehemu
iliyo na ubaridi kidogo na giza.
UTUNZAJI WA KUKU KWA MAKUNDI
Utunzaji wa Vifaranga
Malezi
bora ya vifaranga ni muhimu katika ufugaji wa kuku kwa sababu vifaranga hawana
uwezo wa kustahimili mazingira wakiwa wenyewe mara wanapoanguliwa. Ukosefu wa
malezi bora husababisha vifaranga kuwa dhaifu, kufa kwa wingi na hivyo
kupunguza idadi ya kuku wa baadaye. Malezi ya vifaranga yanaweza kufanyika kwa
kutumia kuku walezi au kutumia vifaa maalum.
Kulea
Vifaranga kwa Kutumia Kuku Mlezi
Vifaranga
wanaweza kulelewa na mama yao au kuku mlezi. Endapo kuku wengi wametotoa
vifaranga kwa wakati mmoja, achaguliwe kuku mlezi aliye na uwezo wa kulea
vifaranga wengi kati ya waliototoa aendelee kulea na wengine waliototoa waachwe
huru ili warudi kwenye mzunguko wa kutaga. Kuku mmoja anaweza kulea vifaranga
20 hadi 25. Mfugaji wa kuku, pamoja na kanuni nyingine, anapaswa kuzingatia
yafuatayo:-
• Kuku anayelea vifaranga
atengewe chumba maalum, apewe maji ya kutosha na chakula chenye virutubishi
muhimu,
• Vifaranga wasiachiwe kutoka nje
hadi watakapofika umri wa wiki 6,
• Vifaranga watengwe na
mama/mlezi baada ya wiki 4 kuruhusu mama aendelee na mzunguko wa kutaga; na
• Katika maeneo yenye hali ya
hewa ya ubaridi vifaranga wacheleweshwe kutenganishwa na mama/malezi hadi wiki
ya 6 au mpaka waonekane wameota manyoya ya kutosha.
Kulea
Vifaranga kwa Kutumia Bruda
Bruda
ni chombo/sehemu iliyoandaliwa mahususi kwa ajili ya kuwapatia joto vifaranga
badala ya mama/mlezi. Mfugaji anaweza kulea vifaranga wengi kwa kutumia bruda
ambayo ni mduara unaoweza kutengenezwa kwa kutumia mbao, karatasi ngumu au kwa
kuziba pembe za chumba. Aidha, njia hii hupunguza vifo vya vifaranga
vinavyosababishwa na ndege au wanyama hatari, huruhusu kuku kutaga mapema zaidi
na kuwa na mizunguko mingi ya utagaji (kwa kuku wanaoatamia). Vilevile,
hurahisisha udhibiti wa magonjwa.
Mfugaji
anapaswa kufuata taratibu zifuatazo katika kulea vifaranga kwa kutumia bruda:-
• Kuweka vifaa vya kuongeza joto
kwa mfano taa ya umeme, chemli au jiko la mkaa. Zingatia kiwango cha joto
katika bruda kinachohitajika. Wiki ya kwanza ni 35 oC,
wiki ya pili ni 33 oC, wiki ya tatu ni 31 oC
na wiki ya nne ni 29 oC,
• Kuchunguza mtawanyiko wa
vifaranga ndani ya bruda ili kutathimini hali ya joto. Wakijikusanya kwenye
chanzo cha joto, inaashiria kuwa baridi imezidi hivyo joto liongezwe. Wakiwa
mbali na chanzo cha joto maana yake joto limezidi hivyo joto lipunguzwe,
• Bruda iwe na sakafu yenye
malalo yatokanayo na maranda ya mbao au pumba za mpunga. Malalo yabadilishwe
endapo yataonekana yameloana,
• Bruda iwekwe vifaa vya maji na
chakula. Maji na chakula kiwekwe kabla ya kuweka vifaranga,
• Vifaa vya joto viwekwe ndani ya
bruda masaa 6 kabla ya kuingia vifaranga,
• Vifaranga walishwe chakula cha
kuanzia gramu 12 - 15 kwa kipindi cha wiki ya kwanza na gram 15 - 21 kwa
kipindi cha wiki ya 2. Katika wiki ya 3 wapewe gramu 21 - 35 kwa kifaranga na
chakula hicho kiwepo muda wote,
• Vifaranga wapatiwe vitamini,
madini na dawa za kinga (antibiotics); na
• Vifaranga wapatiwe chanjo
kulingana na maelekezo ya mtaalamu wa mifugo. Chanjo dhidi ya magonjwa muhimu
kwa mfano, Marek’s (mara anapototolewa), Mdondo (siku ya 3 - 4 na kurudiwa
baada ya siku ya 21 na kila baada ya miezi 3) na Gumboro (siku ya 7 na kurudia
tena siku ya 21). Wapatiwe dawa ya minyoo (wiki ya 8) na Coccidiosis (wiki ya 3
- 4)
Kutunza Kuku Wanaokua (wiki 8 - 18)
Utunzaji
wa kundi hili unategemea mfumo unaotumika.
Kuku
Wanaofugwa Katika Mfumo Huria
Kuku
wanaofugwa katika mfumo huu wapatiwe matunzo bora yakiwemo yafuatayo;
• Wapewe chakula cha ziada
asubuhi kabla ya kutoka na wanaporudi kwenye banda. Chakula hicho kinaweza
kugawanywa mara 2 kwa siku,
• Wapatiwe maji safi na ya
kutosha wakati wote; na
• Wapatiwe chanjo na dawa
kulingana na ushauri wa mtaalam wa mifugo.
Kuku
Wanaofugwa Katika Mfumo Shadidi
• Majogoo watenganishwe na
mitetea katika wiki 7 hadi 10 ili kuzuia uzaliano usio na mpangilio,
• Wapewe chakula cha kukuzia
kuanzia wiki ya 8 - 15 gramu 55 - 60 na kuanzia wiki ya 16 gramu 65 - 80 kwa wanaofugwa
mfumo huria na gram 120- 125 kwa kuku kwa siku kwa wanaofugwa mfumo wa shadidi,
• Kuku wa nyama wapatiwe chakula
cha kuku wa nyama muda wote,
• Wapatiwe maji safi ya kunywa
kwa muda wote kwenye vyombo visafi,
• Kuku wachunguzwe dalili zozote za
ugonjwa ili waweze kupata tiba sahihi kutoka kwa mtaalamu wa mifugo,
• Kuku wa wiki 9 - 20 wanahitaji
nafasi ya mita za mraba 0.15 kwa kuku na wiki 21 au zaidi mita za mraba 0.2 kwa
kuku,
• Kuwe na vyombo maalum vya
kutosha kwa ajili ya chakula na maji
• Wafanyiwe usafi wa banda mara
kwa mara ili kuzuia magonjwa yanayotokana na uchafu; na
• Wakatwe midomo ili kuzuia
kudonoana.
Kuku Wanaotaga
Mahitaji
ya kuku wanaotaga ni tofauti na ya makundi mengine. Mambo ya kuzingatia kwa
kuku wanaotaga ni pamoja na:-
• Banda liwe na viota vya kutagia
mayai (kiota 1 kwa kuku 3 - 5). Viota viwekwe bandani mara kuku watakapofikisha
umri wa wiki 18 ili waanze kuzoea kuvitumia,
• Wapatiwe chakula na maji safi
wakati wote kwa kutumia vyombo maalum ambavyo ni visafi,
• Kuku wasiotaga waondolewe
kwenye kundi. Kuku hao huonekana wasafi na sehemu ya kutolea yai huwa ndogo na
kavu, upanga wake kichwani (comb) huwa mdogo na mwekundu,
• Wapewe dawa ya minyoo kila
baada ya miezi 3,
• Wawekewe fito au ubao mwembamba
kama sehemu ya kupumzikia na mazoezi ili kuzuia kudonoana,
• Mayai yakusanywe mara 4 au
zaidi kwa siku ili yasidonolewe na kuku,
• Kuwe na malalo makavu na
yabadilishwe mara yanapochafuka,
• Vyombo vifanyiwe usafi kila
siku ili kuzuia magonjwa; na
• Watundikiwe majani mabichi aina
ya mchicha, papai, alfaalfa, majani jamii ya mikunde ili kuboresha lishe.
UDHIBITI NA TIBA DHIDI YA MAGONJWA YA KUKU
Kuku
wanaopata lishe bora, kutunzwa vizuri na kupatiwa chanjo dhidi ya magonjwa
yanayotokea mara kwa mara huwa na afya nzuri. Ni bora kuzuia magonjwa kuliko
kutibu ili kupunguza vifo na gharama. Iwapo ugonjwa utatokea kuku wagonjwa
watenganishwe na kuku wasio wagonjwa na wapatiwe tiba. Kanuni muhimu za kufuata
ili kuzuia magonjwa ni:-
• Banda liwe safi muda wote,
• Kabla ya kuweka kuku, banda
linyunyiziwe dawa ya kuua wadudu wa magonjwa mbalimbali,
• Kuku wakaguliwe kila siku ili
kubaini wagonjwa au wenye matatizo, kuwatenga na kutoa taarifa kwa mtaalam wa
mifugo,
• Kuku wapatiwe chanjo dhidi ya
magonjwa mbalimbali,
• Watu wasiohusika wasiingie eneo
la kufugia kuku bila utaratibu,
• Ndege na wanyama wengine
wasifike eneo la kufugia kuku,
• Banda la kufugia kuku
litenganishwe na mabanda ya mifugo mingine,
• Lango la kuingilia katika banda
la kuku liwekewe dawa ya kukanyaga kwa wanaoingia ndani ili kuzuia kuingiza vimelea
vya wadudu wa magonjwa; na
• Vifaa vya chakula na maji viwe
safi wakati wote.
Dalili za Kuku Mgonjwa
Dalili
za ujumla zinazoonekana kwa kuku mgonjwa ni kama zifuatazo:-
• Kuzubaa,
• Kupoteza hamu ya kula,
• Kujitenga na wenzake katika
kundi; na
• Kupunguza au kusimama kutaga.
Mfugaji
anapoona mojawapo ya dalili hizo amwone mtaalam wa mifugo
UFUGAJI WA AINA NYINGINE ZA NDEGE
Aina
ya ndege wengine wanaofugwa hapa nchini ni pamoja na Bata maji, Bata bukini,
Bata mzinga, Kanga na Njiwa. Ndege hao hufugwa kwa kiasi kidogo ukilinganisha
na kuku kwa kuwa soko lao ni dogo. Utunzaji wao hautofautiani sana na kuku;
• Wajengewe banda la kuishi
ambalo ukubwa wake utategemea idadi ya ndege wanaofugwa,
• Wapatiwe chakula chenye
virutubisho na maji ya kunywa ya kutosha,
• Wapatiwe kinga na tiba dhidi ya
magonjwa,
• Bata maji na Bata bukini
wajengewe bwawa lenye nafasi ya kutosha kwa ajili ya kuogelea; na
• Njiwa wajengewe viota sehemu ya
juu kama kwenye mapaa ya nyumba.
UTUNZAJI WA KUMBUKUMBU
Utunzaji
wa kumbukumbu ni muhimu sana katika ufugaji wa kuku na ndege wengine wafugwao
ili kusaidia mfugaji kujua maendeleo ya ufugaji wake. Utaratibu wa kuweka
kumbukumbu mara tukio linapotokea ni lazima ili kuepuka kusahau. Mfugaji
ahakikishe anaweka kumbukumbu ambazo ni sahihi na zinazoeleweka.
Aina za Kumbukumbu
Kumbukumbu zinazopaswa kuwekwa ni
pamoja na:-
• Aina na idadi ya kuku waliopo
kwenye kila kundi (mfano vifaranga, wanaokua, wanaotaga, majogoo),
• Uzalishaji wa mayai kwa kundi
la kuku waliopo,
• Utotoaji wa vifaranga,
• Kinga na matibabu,
• Mapato na matumizi,
• Utagaji wa kila kuku na
utunzaji (kwa kuku wa asili); na
• Kumbukumbu za vifo.
Tumejitahidi kueleza mengi lakini bado mengi mengine, unaweza kubadilishana uzoefu na wafugaji wenzako kwa kuacha comment yako hapa chini
Labels: UFUGAJI, UFUGAJI WA KUKU