Fahamu Kilimo Cha Matango (Cucumber)



Kilimo-cha-matango
Matango huwa tayari kuvunwa kuanzia siku 50 hadi 60, yaani mwezi mmoja na nusu hadi miwili baada ya kupanda, na pia matunda yanatakiwa kuwa na urefu wa sentimita 15 mpaka 20, urefu pia unaweza kutofautiana kulingana na aina ya matango yaliyopandwa.

UTANGULIZI
Asili ya kilimo cha matango inaaminika kuwa ni kaskazini magharibi mwa India ambako yamekuwa yakilimwa kwa zaidi ya miaka thelathini sasa. Hata hivyo kwa sasa, matango, hustawishwa katika sehemu nyingi za kitropiki. Matunda yake hukatwa katwa na kuliwa kama achali, au kachumbari, au huwekwa kwenye siki na pia hupikwa na kuliwa.

Katika nchi yetu ya Tanzania matango hulimwa katika mikoa ifuatayo: Tanga, Morogoro, Mbeya, Lindi, Mtwara na Pwani ambako kuna jua la kutosha. Pia mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kilimo cha matango hukubali.

Aina Za Matango
Zipo aina nyingi za matango lakini hutofautiana kwa umbo na rangi. Aina zinazojulika na kulimwa zaidi hapa kwetu ni: Colorad, Telegraph, Palmetto, Chicago, Pickling, Straight 8 na Marketer.

Matumizi
Matango hutumiwa kama matunda na pia ni aina ya mboga ambayo huongeza vitamin A, C na maji mwilini. Matunda haya yanaweza kutumika pia kama saladi wakati wa mlo.

Matumizi-ya-matango


KUCHAGUA ENEO NA KUANDAA SHAMBA
Eeo linatakiwa liwe na maji ya kutosha na udongo wenye chachu (pH) ya 6.0 hadi 7.5 na hali ya joto wastani wa nyuzi 20 hadi 25 zinahitajika kwa ukuaji bora.  Matango hukua na kukomaa kwa haraka zaidi katika udongo mwepesi, lakini hutoa mavuno makubwa zaidi katika ardhi nzito kiasi. Hata hivyo ardhi inayotuamisha maji haifai kwa kilimo cha matango, na ikibidi mimea ipandwe kwenye matuta.

Kabla ya kupanda udongo unatakiwa utifuliwe vizuri na majani yaondolewe kabisa, usafi bustanini unashauriwa ili kuondoa mimea mingine ambayo inaweza kuwa chanzo cha magonjwa.

Upandaji
Ni vizuri kama mkulima wa matango akapanda mbegu moja kwa moja shambani, sia mbegu moja kiasi cha sentimita moja chini ya udongo, na umbali kati ya mbegu na mbegu usipungue sentimita 30 na zaidi.
Sehemu ya kupandia iwe na jua la kutosha kwani matango huhitaji kiasi cha jua kisichopungua masaa 6 - 8 kwa siku, mwagilia maji ya kutosha angalau mara moja kwa siku hasa nyakati za jioni. Hii itasaidia ukuaji bora wa mazao yako hivyo kukuhakikishia mavuno mazuri.

Nafasi ya kupandia: sm 60 kati ya mimea na sm 90 kati ya mistari.

Mbolea: Kabla ya kupanda weka viganja 2 vya mbolea ya zizi katika kila shimo na changanya na udongo. Pia weka kg 100 za NPK kwa hekta moja. Wiki tatu hadi nne baada ya kupanda: Weka mbolea ya CAN kwa kiwango cha kijiko kimoja cha mezani kwa kila mmea (= gramu 10 kwa mmea). Mbolea ni muhmu sana katika kilimo cha matango kwani zao hili pia hutumia chakula kingi kutoka ardhini, hivyo muhimu kuweka samadi au mboji mara kwa mara ili kuongeza chakula cha mmea.

Palizi
Palilia kila wakati magugu yanapojitokeza, ni muhimu sana, hii husaidia kuepuka magonjwa na kushindania chakula kati ya zao na magugu. Palizi hutakiwa kufanywa kwa kutumia jembe la mkono ili kuepuka kuharibu mizizi.

Matandazo (Mulching)
Baada ya kupalilia na kuweka mbolea weka matandazo (mulch). Mkulima anaweza tumia nyasi au mabaki ya mimea mingine kufunika ardhi, baada ya miche kutambaa kwa kiasi unaweza weka matandazo kwaajili ya kuzuia upotevu wa unyevu, kupunguza uotaji wa magugu na pia matandazo yakioza huongeza rutuba kwenye udongo na hulinda udongo dhidi ya mmomonyoko.

Kita miti (staking) ya kupandia: Chomeka miti ya kupandia matango yanayotambaa. Hii husaidia matango yanayotambaa kupanda kufuata miti uliyoikita/chomeka.

MAGONJWA
Ni magonjwa machache tu yanayoathiri kilimo cha matango, nayo ni:
(a) Mnyauko bacteria (Bacteria Wilt) - hushambulia majani, majani yaliyoshambuliwa hudhoofu na hatimaye hufa. Mmea ukikatwa huchuruzika ute mzito.

Kudhibiti ugonjwa
Nyunyizia dawa ya Copper kila baada ya siku 10 na tumia aina ya mbegu zenye uvumilivu mkubwa kama vile Palmetto.

(b) Ubwiri unga au ukungu (Powdery Mildew) - Ukungu wake hushambulia majani na mashina.
Kudhibiti
Fanya usafi unaohitajika bustanini mfano kuchoma taka. Pulizia Bayfidan.

(c) Magonjwa ya virusi (Cucumber Mosaic Virus) – ugonjwa huu husababishwa na virusi, ikiwa mmea hautatibiwa mapema, mmea hugeuka na kuwa wa njano, hudumaa na hushindwa kutoa matunda. Ugonjwa huu pia huenezwa na magugu au wadudu kama vidukari na inzi weupe.
Kudhibiti
Weka shamba katika hali ya usafi, na upande mbegu zinazovumilia ugonjwa. Nyunyizia dawa ya unga ya sulphur kila baada ya siku 10.

WADUDU
(a) Dudu kobe wa matango - Huyu ni mdudu mbaya sana kwa matango kwani hutafuna miche ya matango mara ichipuapo, pia hushambulia majani ya mimea michanga na kuathiri ukuaji.

(b) Vidukari au wadudu mafuta (Aphids) - wadudu hawa hufyonza utomvu kwenye majani machanga na kudumaza mmea kuufanya ushindwe kuzaa matunda.

Kudhibiti
Inabidi kutumia Malathion, Nicotine. Hakisha dawa inafikia upande wa chini wa majani ili kuhakikisha wadudu wote wamekufa.

(c) Buu au funza (Pickle Worm) - Buu au funza hujipenyeza ndani ya ua, kisha huhamia kwenye tunda.

Kudhibiti
Tumia Rotenone au Crylite kila baada ya juma moja.

Wadudu wengine ni kama minyoo ya mizizi, na inzi weupe

KUVUNA
Matango huwa tayari kuvunwa kuanzia siku 50 hadi 60, yaani mwezi mmoja na nusu hadi miwili baada ya kupanda, na pia matunda yanatakiwa kuwa na urefu wa sentimita 15 mpaka 20, urefu pia unaweza kutofautiana kulingana na aina ya matango yaliyopandwa. Baada ya mvuno wa kwanza mkulima anaweza subiri wiki tatu kabla ya kuvuna mvuno wa pili.

Kuvuna-Matango


Kiasi Cha Mavuno
Ulimaji wa matango unaofuata taratibu tajwa hapo juu hupelekea mavuno ya kiasi cha tani 6 mpaka 10 kwa ekari moja na pia mtango mmoja unaweza zaa matunda matano hadi saba. Hii huweza kutimia endapo mimea itatunzwa vizuri.

Hifadhi
Baada ya kuvuna matango yanatakiwa kuhifadhiwa katika mazingira mazuri yenye kiwango cha unyevu wastani wa 90% hadi 95% na joto wastani nyuzi 10 hadi 13 za centigrade. Chini ya nyuzi joto 10 matango hubadilika rangi na kuwa ya njano hivyo kupunguza ubora wake. Matango yasihifadhiwa kwa zaidi ya siku 14!

SOKO
Matango yana soko kubwa ndani na nje ya nchi yetu. Biashara ya matango ndani ya nchi yanauzwa rejareja kwa bei ya shilingi mia mbili hadi mia tano kwa tango moja. Hata hivo bei hutofautiana kulingana na upatikanaji au uzalishaji wa matango wa mahali husika. Pia unaweza kuuza kwenye migahawa, mahoteli na cafeteria.

Haya ushindwe wewe tu, mwongozo wa kulima matango huo hapo! Ikiwa kuna kitu hujaelewa comment, utajibiwa.

Labels: ,