Mbegu za uyoga huzalishwa kwenye maabara
zenye vifaa vinavyowezesha kuotesha mbegu hizo bila kuchafuliwa au
kuchanganyika na vimelea kama bakteria, ukungu au jamii nyingine za uyoga
ambazo haziliwi. Hapa Tanzania hivi sasa maabara hizo zipo Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kituo cha utafiti wa
kilimo-Uyolena taasisi ya utafiti wa kilimo cha bustani- Tengeru (HORTI –
Tengeru, Arusha).
Utangulizi
Miaka ya
karibuni, utaalamu wa kilimo cha uyoga umeanza hapa Tanzania baada ya watu
kutilia maanani lishe bora ya protini na manufaa mengine ya zao hilo. Kwa kuwa
uyoga upo wa aina mbalimbali, usitawishaji wake hutofautiana katika mahitaji
yake, ikiwa ni pamoja na hali ya hewa, malighafi za kuoteshea, urahisi wa
teknologia ya kuotesha katika mazingira ya Tanzania na soko lake kwa wananchi
na katika hotel. Hata hivyo ni wananchi wachache tu wanaojua kilimo cha uyoga.
Uyoga unaozalishwa unafahamika. Aina zinazofaa kwa Tanzania ni zile ambazo
hustawi vizuri, kwenye maeneo ya joto la wastani wa nyuzi joto 20C hadi 33C.
Kwa
mfano uyoga aina ya mamama (Oyster mushrooms, Pleurotus spp.), uyoga wa
vifundo (Agaricus), uyoga taka (Coprinus) n.k. Aina hizi za uyoga
pia huhitaji hali ya unyevu hewani kiasi cha asilimia 75%. Oyster mushroom ni
maarufu zaidi hapa Tanzania.
Namna Ya
Kuotesha Uyoga
Kabla
ya kuanza kuzalisha uyoga inabidi kuwa na chumba chenye paa ambalo litazuia
jua, mvua, na vumbi. Chumba hiki kinatakiwa kiwe na sakafu inayohifadhi
unyevunyevu pamoja na sehemu ya giza ambayo ni muhimu kwa kuotesha utando wa
uyoga. Mkulima wa kawaida anaweza kutumia kasha kama sehemu ya giza.
Mbegu
za uyoga huzalishwa kwenye maabara zenye vifaa vinavyowezesha kuotesha mbegu
hizo bila kuchafuliwa au kuchanganyika na vimelea kama bakteria, ukungu au
jamii nyingine za uyoga ambazo haziliwi. Hapa Tanzania hivi sasa maabara hizo
zipo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
kituo cha utafiti wa kilimo-Uyolena taasisi ya utafiti wa kilimo cha bustani-
Tengeru (HORTI – Tengeru, Arusha).
Hatua Muhimu Katika Kuotesha Uyoga
Hatua
muhimu za kuotesha uyoga baada ya kupata mbegu ni kama ifuatavyo:
• Kusanya masalia ya mzao kama vile mabua,
majani ya mpunga, ngano, pumba za mpunga au mahindi, masalia ya miwa baada ya
kukamua nk. Vitu hivi hutumika kama mali ghafi kwa kuoteshea uyoga.
• Mabua, majani ya mpunga au migomba yakatwe kwa
urefu usiozidi sm 6, au urefu wa vidole kwa kutumia panga au kisu.
• Loweka mali ghafi kwenye maji ya kawaida kwa
muda wa siku nzima (saa 24).
• Kisha yachemshe kwa muda wa saa mbili ili kuua
vijidudu pamoja na vimelea vilivyomo.
• Ipua na umwage maji yote halafu tandaza kwenye
kichanja kisafi ili yapoe bila kuchafuliwa na vumbi au vijidudu.
• Kisha
jaza mali ghafi hii katika mifuko ya nailoni tayari kwa kupanda mbegu.
Namana ya kupanda
Kuna aina mbili za upandaji:
*Aina ya kwanza: Chukua mfuko wa nailoni wenye upana wa sm 40 - 45 na kimo sm 75. Weka
tabaka ya mali ghafi ya kuoteshea yenye kina cha sm 10 katika mfuko halafu
tawanya mbegu ya uyoga juu yake.
Baada ya kuweka mbegu, weka tena tabaka nyingine ya
vioteshea na kuweka mbegu juu yake. Endelea kuongeza tabaka kwa namna hii mpaka
ifike ujazo wa robo tatu ya mfuko.
*Aina ya pili: Changanya malighafi ya kuoteshea (baada ya
kuchemshwa na kupoa) na mbegu ya uyoga katika uwiano wa 1: 25 (mbegu : mali ghafi
ya kuoteshea) kwa uyoga aina ya mamama (Pleurotus spp.). Kisha
mchanganyiko huo ujazwe katika mifuko ya nailoni, mifuko hii iwe na ukubwa wa
sm 20 kwa sm sm 40 ambamo unaweza kujaza kilo 1 - 11/2 ya mali ghafi ya
kuoteshea. Funga mifuko na toboa matundu kwenye mifuko yenye kipenyo cha sm 1
kwa kila umbali wa sm 6 hadi 10 kwa kila mfuko.
Zingatia: Matundu yawe mengi ili kuingiza hewa ya kutosha
ndani ya mifuko. Kumbuka uyoga ni kiumbe hai hivyo unahitaji kupumua.
Matunzo Ya Zao La Uyoga
Weka mifuko kwenye chumba cha giza. Kwa mkulima wa
kawaida waweza kutumia kasha lisilopitisha mwanga kama chumba cha giza. Acha
mifuko humo kwa muda wa siku 14 - 21 bila kufunua ili ukungu mweupe uweze
kutanda vizuri.
Utando wa uyoga ukishatanda vizuri kwenye malighafi ya kuoteshea, hamishia kwenye chumba chenye mwanga na hewa ya kutosha
kisicho pigwa na jua. Katika chumba chenye mwanga, mifuko inaweza kuwekwa kwenye,
meza, chanja la waya au miti. Mifuko inaweza pia kuning’inizwa kwenye kamba
toka kwenye boriti.
Zingatia: Unatakiwa kudumisha hali ya unyevu kwenye chumba
hicho cha mwanga kwa kumwaga maji sakafuni. Ukiona vipando vinakauka unaweza
kunyunyizia maji yaliyochemshwa na kupoa juu ya mifuko mara tatu au zaidi kwa
siku. Tumia bomba la mkononi lenye ukubwa wa lita moja kunyunyizia maji.
Tahadhali: Usizidishe maji
kwani maji yakiwa mengi sana yaweza kuozesha uyoga uliyoanza kuota. Aina nyingi
za uyoga huanza kutoa vichwa (pini) siku 2 - 3 baada ya kuwekwa kwenye mwanga.
Uvunaji Wa Uyoga
Uyoga huwa tayari kuchumwa siku tatu baada ya
vichwa /pini kuonekana. Uyoga uvunwe kwa mkono kwa kushika katikati ya shina la
uyoga kisha zungusha hadi uyoga ung’oke. Usiondoe kichwa peke yake katika
kuvuna uyoga kwani kubakiza shina huzuia uyoga mwingine kutokea.
Zingatia: Mkulima
anatakiwa ajue soko la uyoga kabla ya kuvuna ili kuepuka gharama za kuhifadhi. Kwani
uyoga ukishavunwa unatakiwa uliwe kabla haujaharibika.
Jinsi ya kuhifadhi uyoga
i) Unaweza ukauweka uyoga kwenye mifuko ya karatasi
na kuhifadhi kwenye jokofu.
ii) Unaweza ukauanika juani hadi ukauke na kuweka
kwenye mifuko ya nailoni iliyofungwa vizuri ili isipitishe hewa na unyevu.
Soko La Uyoga
i) Watu wengi hupenda uyoga mbichi uliotoka
shambani wakati huo huo kama kitoweo, kwa kutumia kama nyama, samaki, au kama
kiungo.
ii) Unaweza kuuza uyoga mbichi kwa bei ya shilingi
3000/= hadi 5000/= kwa kilo kwa uyoga aina ya mamama. Pia waweza kuuza nje ya
nchi ikiwa uyoga wako ni kiasi kikubwa na uko katika viwango vinavyo kubalika
kimataifa.
Mambo Ya Kuzingatia
• Uzalishaji wa uyoga huzingatia sana hali ya hewa
na vifaa ulivyonavyo, hivyo basi, kabla hujachagua aina ya uyoga unaotaka
kupanda pata ushauri kwa wataalamu walio karibu nawe.
• Ukishanunua mbegu, kama hupandi kwa muda huo, hakikisha
umehifadhi mbegu hiyo kwenye jokofu. Kama huna jokofu la kuhifadhia, nunua
mbegu baada ya kuandaa kila kitu. Hata hivyo, uotaji wa mbegu huwa mzuri kama
zitakaa nje ya jokofu kwa siku mbili.
• Mbegu za uyoga huwekwa ndani ya chupa yenye ujazo
wa mililita 300, waweza kutumia chupa moja katika kupanda kwenye kilo 15 ya
mali ghafi ya kuoteshea. Hakikisha unamaliza mbegu yote iliyo ndani ya chupa
kwani ikibaki itapata maambukizo ya vimelea.
• Hakikisha unaponunua mbegu iwe ni nyeupe. Mbegu ambayo
siyo nyeupe ni dalili za maambukizo ya vimelea vingine na hivyo haifai kwa
kupanda.
• Hakikisha chumba cha kupandia ni kisafi na
hakipati vumbi toka nje ili kuzuia maambukizo ya magonjwa ya uyoga.
• Usimwagilie uyoga maji yasiyochemshwa kwani maji
hayo mara nyingi si salama. Yaweza kusababisha vimelea vingine kuota, kwani
uyoga ni dhaifu kuhimili ushindani wa vimelea.
• Pia waweza kusababisha magonjwa ya uyoga ambayo kutibu
kwake kunahitaji kutumia dawa za viwandani ambazo ni sumu na hivyo kusababisha
madhara kwa mlaji.
Unaweza kupata
faida nyingi kutokana na uzalishaji wa uyoga, faida hizo ni kama zifuatazo:-
• Lishe kama protini inayolingana na ile
ipatikanayo kwenye maziwa, samaki na kunde. Pia utapata vitamini B, C, na D, na
madini ya joto, phosphoras, chuma na potashi.
• Uyoga husadikika kutibu maradhi kama kifua kikuu,
kisukari, moyo, shinikizo la damu na figo.
• Masalia ya mazao hutumika katika kuzalishia uyoga,
na baadaye yanaweza kutumika kama mbolea asili kwa kilimo cha bustani. Masalia
ya kilimo cha uyoga pia hutumika kama chakula cha mifugo kama ng’ombe.
• Kilimo hiki huhitaji eneo dogo sana la ardhi na
kiasi kidogo cha maji, hivyo hupunguza tatizo la ukosefu wa ardhi na ugomvi
katika jamii ambao unatokana na tatizo hilo.
• Kilimo cha hiki cha uyoga ni njia nyepesi ya
kutoa ajira kwa familia kutokana na gharama ndogo, teknolojia rahisi inayotumika
na pato lake kubwa.
Je kuna kitu hujaelewa? Comment hapo chini
Labels: KILIMO BORA, KILIMO CHA UYOGA