Ufugaji wa kuku ni nyenzo
nzuri ya kujipatia kipato katika kaya kwa sababu hauhitaji
mtaji mkubwa na hauna kazi kubwa kiuendeshaji. Katika ufugaji huria kuku
hujitafutia chakula wenyewe.
UTANGULIZI
Ufugaji wa kuku ni nyenzo nzuri ya kujipatia kipato katika kaya kwa sababu ufugaji wa kuku hauhitaji mtaji mkubwa na hauna kazi kubwa kiuendeshaji. Katika ufugaji huria kuku hujitafutia chakula wenyewe. Pia inapowezekana hupewa mabaki ya chakula,
chenga, pumba au nafaka yoyote inayopatikana katika mazingira husika. Kwa walio
wengi ifikapo nyakati za jioni, kuku hulala jikoni au ndani nyumbani kwa
mfugaji mwenyewe. Ufugaji huu ni rahisi kwa kuwa hauna gharama kubwa ila faida
yake ni kitoweo tu au fedha kidogo sana.
Tanzania ina idadi ya kuku wa
kienyeji wanaokadiriwa kuwa million 34 ambao wanafugwa kwa mtindo wa huria.
Ufugaji wa aina hii hufanyika vijijini na mijini pia. Idadi hii ya kuku bado ni
ndogo ikilinganishwa na mahitaji halisi ya Watanzania wanaokadiriwa kuwa
milioni 40 (sensa ya mwaka ---). Ulaji wa nyama ya kuku nchini unakadiriwa kuwa
ni wastani wa kilo 0.7 kwa kila mtu kwa mwaka mzima ilihali Shirika la Chakula
na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) linakadiria wastani mzuri wa ulaji wa nyama
kuwa ni kilo 6.8 kwa mtu kwa mwaka. Hii inaashiria kuwa soko la kuku nchini ni
kubwa, ambayo ni fursa muhimu kwa wafugaji wa kuku.
Kutokana na lishe duni na
kuzaana wenyewe kwa wenyewe (bila kubadili jogoo), kuku wa kienyeji walio wengi
wana uzito mdogo. Wana wastani wa uzito wa robo tatu za kilo hadi kilo moja
wakiwa na umri wa zaidi ya mwaka mmoja. Ila wakitunzwa vizuri zaidi na
kuboreshwa wana uwezo wa kufikia uzito wa kilo moja hadi moja na nusu katika
umri wa miezi sita hadi nane.
Kwa upande wa utagaji wa mayai
kuku wa kienyeji kwa wastani hutaga mayai 50 hadi 65 kwa mwaka. Wakitunzwa
vizuri zaidi huweza kufikia uzalishaji wa mayai 80 hadi 100 kwa mwaka.
Mambo yanayomfanya
mfugaji kuamua atumie njia fulani ya kufuga ni pamoja na uwezo wa kugharamia
shughuli ya ufugaji wa kuku na ukubwa wa eneo alilonalo la kufugia. Katika
sehemu hii utajifunza njia tatu za kufuga kuku ambazo ni:
1. Kufuga huria
Kuku huachwa
wenyewe kujitafutia chakula na maji. Njia hii inatumika zaidi kufuga kuku wa
kienyeji. Mara chache sana mfugaji huwapatia kuku chakula cha ziada. Kwa
ufugaji huu lazima kuwe na eneo kubwa la kutosha kuku kuzunguka na kutafuta
chakula. Kuku hulala eneo lisilo rasmi kama vile jikoni, kwenye kiambata n.k.
Faida zake
• Ni njia rahisi
ya kufuga.
• Gharama yake pia
ni ndogo.
• Kuku wanapata
mazoezi ya kutosha.
• Kuku wanapata
chakula mchanganyiko ambacho kinafaa kiafya.
Hasara zake
• Kuku huwa
hatarini kuibiwa au kudhurika na wanyama wakali na hali mbaya ya hewa.
• Ukuaji wa kuku
ni hafifu, hufikia uzito wa kilo 1.2 baada ya mwaka.
• Huharibu
mazingira kama kula na mimea ya bustanini mazao kama nafaka.
• Ni rahisi
kuambukizwa magonjwa.
2. Kufuga nusu
ndani – nusu nje
Huu ni mtindo wa
kufuga ambapo kuku wanakuwa na banda lililounganishwa na uzio kwa upande wa
mbele. Hapa kuku wanaweza kushinda ndani ya banda au nje ya banda wakiwa ndani
ya uzio. Wakati wa mchana
kuku huwa huru kushinda ndani ya banda hasa wanapotaka kutaga na wakati wa
kuatamia au wanaweza kukaa ndani ya uzio nje.
Faida za kufuga nusu
ndani na nusu nje
• Kuku wanakuwa
salama mbali na maadui mbali mbali.
• Utaweza
kuwalisha kuku wako vizuri hivyo wataweza kuongeza uzalishaji wa mayai na wa
nyama (kwa kukua haraka).
• Itakuwa rahisi
kwako kudhibiti wadudu na vimelea vinavyoweza kuleta magonjwa kwa kuku wako.
• Ni rahisi
kuwatenganisha kuku katika makundi tofauti na kuwahudumia ipasavyo.
• Ni rahisi
kutambua kuku wagonjwa kuliko kufuga huria.
• Kuku watapata
mwanga wa jua wa kutosha pamoja na hewa safi.Wakati wa jua kali watakuwa huru
kuingia ndani ya banda na kukaa kivulini.
• Kuku hawatafanya
huharibifu wa mazao yako shambani au bustanini na kwa majirani zako.
• Utapata urahisi
wa kukusanya na kupeleka mbolea bustanini au shambani.
Changamoto ya kufuga
nusu ndani na nusu nje
• Huna budi uwe na
muda wa kutosha kwa ajili ya kuwahudumia kuku wako.
• Pia utahitaji
kuwa na eneo kubwa kiasi la kufugia.
• Pia utaingia gharama
ya ziada kidogo ya kutengeneza banda na wigo na kuwapatia uku chakula cha
ziada.
• Hata hivyo
gharama za muda huo na za vifaa vingine zitafidiwa na mapato ya ziada
utakayopata kwa kufuga kwa njia hii.
3. Kufuga ndani ya
Banda tu
Njia nyingine ni
kuwafuga kuku ndani tu. Katika njia hii, kuku hukaa ndani wakati wote. Njia hii
ya ufugaji utumiwa zaidi na wafugaji wa kuku wa kisasa. Lakini yaweza kutumika
hata kwa kuku wa asili hasa katika sehemu zenye ufinyu wa maeneo.
Changamoto za ufugaji
wa ndani ya banda tu
• Unatakiwa uwe na
muda wa kutosha wa kuwahudumia kuku wako kikamilifu.
• Pia unatakiwa
kuwa na mtaji mkubwa wa kujenga banda na kuwanunulia kuku chakula.
• Ugonjwa ukiingia
na rahisi kuambukizana.Vilevile kuku huweza kuanza tabia mbaya kama kudonoana,
n.k.
Faida za kufuga ndani
tu
• Ni rahisi
kutambua na kudhibiti magonjwa.
• Ni rahisi
kudhibiti upotevu wa kuku, mayai na vifaranga.
• Ni rahisi
kuwapatia chakula kulingana na mahitaji ya kila kundi.
• Ni rahisi
kuwatambua na kuwaondoa kuku wasiozalisha katika kundi.
Ni ufugaji upi unafaa
zaidi kutumika kwenye mazingira ya vijijini?
Kwa ujumla, njia
rahisi na inayopendekezwa kutumiwa na mfugaji wa kawaida kijijini ni ya ufugaji
wa nusu ndani na nusu nje, yaani nusu huria. Hii inatokana na faida zake kama
zilizoainishwa hapo awali. Kwa kutumia mfumo huu wa ufugaji, utaepuka hasara za
kufuga kwa mtindo wa huria kama zilivyainishwa mwanzoni mwa makala hii. Pia
ukitumia mtindo wa ufugaji wa nusu huria utafanya ufugaji wako kwa njia bora
zaidi ndani ya uwezo ulionao, kwa sababu kwa sehemu kubwa utatumia mali ghafi
inayopatikana katika eneo lako.
Sifa za banda bora
la Kuku
Ukiamua kufuga
katika banda kwa njia mbili zilizoelezwa awali utatakiwa kujenga banda lenye sifa
zitakazokidhi mahitaji ya msingi ya kuku. Banda bora la kuku linatakiwa kuwa
kama ifuatavyo:
i) Liwe jengo imara
• Pasiwe na sehemu
zilizo wazi kwenye msingi na kati ya ukuta na paa.
• Banda lijengwe
na vifaa vinavyopatikana katika mazingira yako ili liwe na gharama utakayoweza kumudu.
• Unaweza kutumia
matofali ya udongo, udongo, miti, fito,n.k. Ukitumia fito au mabanzi ondoa
maganda ili kuthibiti mchwa.
• Jengo mara
litazuia maadui kama panya, vicheche, paka, nyoka na wezi kuingia ndani ya
banda na kuwadhuru au kuwaiba kuku.
ii) Liwe rahisi kusafisha
• Kuta na sakafu
visiribwe zisiwe na nyufa ili kurahisisha kusafisha.
• Pia itadhibiti
kusiwe na wadudu wa kujificha katika nyufa kama papasi, viroboto n.k.
• Sakafu ya banda
lazima iwekewe matandazo kama pumba ya mpunga au Maranda ya mbao au mabaki ya
mazao au nyasi kavu kutegemeana na kinachopatikana kwa urahisi katika mazingira
yako.
• Matandazo haya
husaidia kunyonya unyevu unaotokana na kinyesi cha kuku au maji yanayomwagika
katika banda.
• Banda hubakia
kavu bila kuwa na harufu mbaya na wadudu kama inzi hata vimelea vya magonjwa
hudhibitiwa.
iii) Eneo la nje kuzunguka
banda kuwe na usafi wa kudumu
Hali ya usafi nje
ya banda itafanya wadudu kama siafu au mchwa na wanyama kama panya na paka
mwitu wakose maficho. Nje ya banda ndani ya uzio kuwe na miti midogo na mimea
mingine midogo kwa ajili ya kivuli.
iv) Liwe na nafasi ya
kutosha kwa kuku waliopo: Kwa kawaida eneo la mita mraba moja hutosha kuku wanne wanaotaga au
kuku 8 wa nyama. Nafasi ya mita
mraba 1 inatosha vifaranga 16 hadi kufikia umri wa majuma manne.
v) Liweze kuingiza hewa
na mwanga wa kutosha: Banda linaloweza kuingiza hewa safi na kutoka ndani yake hubaki kavu.
Harufu mbaya hutoka na kuku huweza kupumua hewa safi. Hii husaidia pia
kudhibiti kuzaliana kwa vimelea vinavyosababisha magonjwa,hivyo hudhibiti
magonjwa.
vi) Lisiwe na joto sana
au baridi sana: Panda miti ya
kuzunguka banda lako ili eneo liwe na kivuli cha kutosha na pia lisiwe na upepo
mkali.Kama hali halisi ya eneo la kufugia ina joto kubwa kwa vipindi virefu paa
la banda wakati wa ujenzi liinuliwe juu zaidi kuruhusu mzunguko zaidi wa hewa
na joto la paa (kama ni la bati) liwe mbali juu ya kuku. Joto kwenye banda
linaweza kusababishwa na msongamano wa kuku, hivyo mfugaji aangalie aweke idadi
ya kuku inayowiana na ukubwa wa banda lake.
vi) Paa
Liwe imara na lisilovuja.
Waweza kutumia mabati, nyasi, madebe, makuti n.k. kutegemeana na upatikanaji wa
vifaa vya kuezekea.Wakati wa kuezeka paa lisiishie karibu sana na ukuta bali liwe
na sehemu kubwa iliyozidi ukuta kuzuia mvua kuingia ndani kama ni ya upepo (
angalia mchoro hapa chini).
Vifaa vinavyohitajika
katika banda la kuku
Kuku wakifugwa kwa
mtindo wa nusu ndani na nusu nje wanahitaji huduma mbalimbali ndani ya banda na
ndani ya wigo. Ili kutoa huduma hizi vifaa vifuatavyo ni muhimu view katika
banda:
i) Vyombo vya Maji
Kuna njia nyingi
za kutengeneza vyombo vya kuwekea maji ya kuku ya kunywa.
• Aina ya mojawapo
unayoweza kutumia ndoo au debe la lita kumi au ishirini ya plastiki. Kata ndoo
hiyo pande nne kutoa nafasi ya kuku ya kunywea kama kielelezo kinavyoonyesha.
Tengeneza idadi ya vyombo hivi inayowiana na wingi wa kuku ulionao.
• Au waweza
kutumia sufuria au beseni pana kiasi. Hii huwekewa tofali au jiwe safi pana
baada ya kuwekewa maji ya kunywa ili kuzuia kuku wadogo wasizame na maji yasichafi
liwe kirahisi.
• Vifaa maalum vya
kunyweshea kuku vinapatikana katika maduka ya pembejeo za kilimo.
ii) Vyombo vya Chakula
Vyombo hivi ni
muhimu viwe vimetengenezwa vizuri ili visiwe chanzo cha upoteaji wa chakula. Unapotengeneza
kilishio cha kuku kumbuka kuwa kuku wana tabia ya kuchakura. Husambaza au
kupekua chakula kwa miguu hata kwa midomo ili kupata chakula cha chini. Tabia
hii husababisha kumwagwa kwa chakula kingi chini na kusababisha hasara. Unaweza
kudhibiti tatizo hili kwa kutengeneza vyombo visivyoruhusu kuku kuchakura kama
inavyoonyeshwa kwenye kielelezo hapa chini.
Unaweza
kutengeneza kilishio hiki wewe mwenyewe au fundi seremala waliopo katika eneo
unaloishi. Inafaa kilishio kiwe chembamba ili kuku wasiweze kuingia. Pia
kinatakiwa kiwe kirefu ili kuku waweze kula bila kusongamana.
iii) Viota
Zipo aina tofauti
za viota ambazo hutumika kwa ajili ya kutagia. Ipo aina ya ambayo ni ya kutagia
kuku mmoja mmoja. Vipimo vinavyopendekezwa kwa kila kiota ni upana wa sentimita
30, urefu sentimita 30 na kina sentimita 35. Upande wa mbele uachwe wazi ila
sentimita 10 za kwanza kutoka chini zizibwe na ubao (angalia kielelezo). Weka
idadi ya viota inayotosheleza kuku ulio nao.
Pia ipo aina nyingine
inayoweza kutumiwa na kuku zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja. Ni kama kiota kimoja
kilichogawanywa katika vyumba kadhaa. Ila kila chumba kina vipimo kama vya kiota
kimoja (angalia picha hapa chini). Aina hii ya kiota ina upana wa sentimita 30
na kina sentimeta 35 na urefu wake unategemea idadi ya viota. Viota vinatakiwa
kuwa na giza ili kuku wasiogope kuingia kutaga ndani yake. Pia giza husaidia
kupunguza tabia ya kuku kula mayai na kudonoana. Kiota kinafaa kuwekwa mahali
ambako ni rahisi kuku kuingia na kutoka. Vile vile iwe ni sehemu
itakayorahisisha usafishaji wa kiota chenyewe.
iv) Vichanja
Kuku wana asili ya
kupenda kulala au kupumzika sehemu iliyoinuka. Hivyo ndani ya banda weka
vichanja vitakavyotosheleza idadi ya kuku waliopo.
SOMA: Ufugaji wa kuku wa kienyeji - Part 2
Labels: UFUGAJI, UFUGAJI WA KUKU