Vitunguu - Kilimo na Hifadhi bora. Part 1



1. UTANGULIZI
Vitunguu ni zao muhimu sana hapa Tanzania. Mikoa ya Arusha, Manyara, Iringa, Mbeya, Tanga, Singida na Kilimanjaro ni maarufu sana kwa kilimo cha vitunguu na ni zao la chakula na biashara kwa mkulima mdogo.
Morogoro, Iringa (wilaya ya Kilolo mpakani mwa mkoa wa Morogoro) na kwenye maeneo ya mto Ruaha, Mara , Morogoro wilayani Kilosa sehemu za Lumuma na Malolo, pia ni maarufu kwa kilimo hiki.
Uzalishaji wa vitunguu bado ni mdogo (tani nne kwa hekta) na upotevu wa mazao baada ya kuvuna ni mkubwa (50 %– 80%) kutokana na hifadhi duni hivyo wakulima wanahitaji utaalamu wa kilimo bora na hifadhi ya vitunguu ili kuongeza uzalishaji na kipato.

2.0 UZALISHAJI WA VITUNGUU
Zao la vitunguu linazalishwa kutokana na mbegu na miche inakuzwa kwenye kitalu kabla ya kupandikizawa shamban. Miche inakuwa na kuzaa vitunguu.Vitunguu vikikomaa, vinavunwa na kuhifadhiwa vikiwa katika hali ya kulala bwete. Katika hali hii vitunguu vinaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu aitha kwa ajili ya kuzalisha mbegu msimu unaofuata au kuuza. Wingi na ubora wa zao la vitunguu hutegemea; hali ya hewa, aina ya vitunguu, upatikanaji wa mbegu bora, kilimo bora, uangalifu wakati wa kuvuna, usafirishaji na hifadhi bora.

2.1 UZALISHAJI
Hali ya hewa na maji
Hali ya hewa na maji ni vipengele muhimu sana vya kuzingatia katika uzalishaji wa vitunguu. Vitunguu vinastawi vizuri katika hali ya ukavu kwa kutumia umwagiliaji. Maji mengi hasa wakati wa masika inasababisha magonjwa mengi hasa ukungu, vitunguu haviwezi kukomaa vizuri, hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa mazao. Jua na hewa kavu ni muhimu sana wakati wa kukomaa na kuvuna vitunguu.
Shamba la vitunguu vilivyostawi

Aina za vitunguu
Aina bora za vitunguu ni pamoja na Mang’ola red, Red creole na Bombay Red. Hizi ni mbegu bora ambazo zinatoa mazao mengi kuanzia 40-60kgs kwa hekta ikiwa kilimo bora kitazingatiwa. Aina zingine za vitunguu ni pamoja na Tropical Red F1 hybrid, Singida local na Pretoria Grano.

Mkulima anaweza kuchagua mbegu kwa kuzingatia:-
Red creole
· Mahitaji ya soko (vitunguu vyekundu hupendwa zaidi)
· Musimu wa kupanda
Bombay Red
· Uwezo wa kuzaa mazao mengi
· Uwezo wa vitunguu kuhifadhiwa kwa muda mrefu.






Mbegu bora
Ubora wa mbegu ni muhimu sana, kwani ndiyo chanzo cha mazao bora. Mbegu bora inatoa miche yenye afya na kuzaa mazao mengi na bora. Mbegu za vitunguu inapoteza uoto wake upesi baada ya kuvunwa (mwaka 1). 
Mbegu nzuri zina sifa zifuatazo:-
· Uotaji zaidi ya 80%
· Mbegu safi zisiyo na mchanganyhiko
· Zimefungwa vizuri kwenye vyombo visivyopitisha hewa na unjevu.

Hivyo mkulima anaponunua mbegu za vitunguu azingatie yafuatayo:
· Chanzo cha mbegu
· Tarehe ya uzalishaji
Mbegu ya vitunguu
· Tarehe ya kuisha muda wake
· Kifungashio cha mbegu.

Inashauriwa mkulima asipande mbegu zenye umri zaidi ya mwaka mmoja.
Mbegu bora za vitunguu zinauzwa na makampuni binafsi kama: ALPHA Seed Co., Popvriend,
Rotian Seed, Kibo Seed, East African Seed Company nk. Wasambazaji wa mbegu ni pamoja na maduka ya TFA, na maduka ya bembejeo za kilimo katika maduka mbalimbali.



Jinsi ya kuandaa kitalu na kuzalisha miche
· Sehemu ya kitalu iwe wazi, mbali na kivuli na kiwe karibu na chanzo cha maji.
· Tengeneza tuta la kubwa wa 1m x 2m . Urefu na idadi ya matuta hutegemea kiasi cha mbegu. Kiasi cha mbegu kwa hectare moja ni kilo 6 au 2 kg kwa eka. 
· Weka samadi iliyooza vizuri kiasi cha debe moja au mchanganyiko wa mbolea ya TSP na CAN (200gm) kwa uwiano wa 1:1 kwenye tuta changanya vizuri na udongo.
· Sia mbegu kwenye mistari kwa nafasi ya 1 sm x 20 sm. Tawanya mbegu vizuri wakati wa kusia ili miche isisongamane.
· Funika mbegu na weka matandazo ya nyasi kavu juu ya tuta na mwagiliwa maji. Udongo unatakiwa kuwa na unyevu kiasi mpaka mbegu ziote.
· Nyasi ziondolewe mara tu mbegu zikiota (siku7-10 kutegemea hali ya hewa).
· Miche itunzwe vizuri na kitalu kiwe katika hali ya usafi.
· Miche imwagiliwe maji mpaka ifikie umri wa kupandikiza shambani (wiki 5-6)
Kitalu cha mbegu ya vitunguu
Matatizo ya miche kitaluni ni kama yafuatayo:
Kuonza kwa mbegu, kunyauka kwa miche kabla na baada ya kuoto. Hali hii inasababishwa na ugonjwa wa ukungu “Kinyausi” .Dawa za ukungu kama Dithane M45 au Ridomil MZnk zinatumike kuzuia (changanya dawa na povu la sabuni ili dawa ijishike kwenye majani). Pia uangalifu uwepo wakati wa kumwagilia maji. Mwagilia maji wakati wa asubuhi au jioni.
Kitalu kilichoathiiriwa na kinyausi (damping off)
Epuka:
Kumwagilia maji wakati wa jua kali kwani unjevunjevu hewani unaongeza na kusababisha vimelea vya magonjwa.

Wadudu waharibifu ni pamoja na Chawa wekundu ambao wanashambulia majani, Sota ambao hukata miche. Dawa za viwandani kama Thiodan , Selecron au Dusrban zinazuia na kudhibiti hawa wadudu. Baada ya wiki 5 au 6, kutegemeana na hali ya hewa miche itakuwa tayari kupandikiza shambani. Miche iimarishwe kwa kusitisha maji, wiki moja kabla ya kupandikiza.

Kutayarisha shamba
Shamba litayarishwe sehemu usiyokuwa na mwinuko, sehemu ya wazi ambayo haijalimwa vitunguu kwa muda wa miaka 2 -3. Shamba liwe karibu na chanzo cha maji kwa ajili ya umwagiliaji. Matuta 1m x 3m au majaruba ya 2mx 3m.yanafaa kwa kupanda miche. Matatu au majaruba yanarahisisha umwagiliaji, palizi na unyunyiziaji wa dawa.

Kupandikiza miche shambani na matumizi ya mbolea
Upandaji wa miche ya vitunguu
Weka samadi debe 2 au mbolea ya TSP au DAP kwenye tuta au jaruba na kuchanganya na udongo. Mbolea kiasi cha mifuko 2 TSP au DAP kwa hekta au ¾ mfuko kwa eka moja inashauriwa. Chagua miche yenye afya, majani na mizizi ya ipunguzwe ili kurahisisha upandaji. Panda miche kwenye mistari kwa nafasi ya sm 20 toka mstari hadi mstari, na miche hadi mche kwa nafasi ya sm 8 au sm 10. Tumia kijiti au kitu chochote chenye ncha kuchimba vijishimo vya kupandia miche. Mwagilia maji ya kutosha kila siku hasa sehemu zenye jua kali. Mbolea ya kukuzia CAN kiasi cha mifuko 2 kwa hekta au ¾ mfuko kwa eka moja iwekwe wiki mbili baada ya kupandikiza miche. Matumizi ya mbolea ya CAN yanataka uangalifu sana. Mbolea ikizidi hufanya mimea kuwa teketeke, shingo ya vitunguu kuwa nene, kuchelewesha kukoma na kupunguza mazao na ubora wa vitunguu. Pia kuoza kwa vitunguu ghalani kunaongezeka
Miche ya vitunguu baada ya kupandikizwa
Kuzuia magugu
Miche ya vitungguu, huota taratibu sana, hivyo miezi ya mwanzoni, miche husongwa sana na magugu. Palizi mbili mpaka tatu zinashauriwa na zinatosha kuweka shamba safi. Matumizi ya dawa za magugu ni madogo lakini dawa zinazoshauriwa ni pamoja na Alachlor na Oxyflourfen (Goal 2E). Hizi dawa ni nzuri kwani zina uwezo wa kuua magugu aina mbalimbali. Dawa inapuliziwa wiki mbili mpaka tatu baada ya kupandikiza miche shambani. Palizi baada ya kutumia dawa ya magugu ni muhimu ili kuondoa magugu sugu na pia kutifulia vitunguu. Wakati wa palizi, vitunguu na mizizi iliyowazi ifunikwe kwa udongo ili kuzuia jua lisiunguze mizizi au kubabua vitunguu.
Shamba la vitunguu
2.2 MAGONJWA NA WADUDU WAHARIBIFU
                    Soma hapa

Soma KILIMO CHA VITUNGUU Part 2


Labels: