3.0 KUVUNA NA
HIFADHI YA VITUNGUU
Kabla ya kuvuna
vitunguu kagua shamba ili kuhakikisha kuwa vitunguu vimekomaa.
Dalili ya
vitunguu kukomaa ni:-
· Majani
kunyauka na kuanza kukauka
· Asilimia 75
-100% kuangusha shingo na majani kukauka.
3.1 KUVUNA
Viitunguu huweza
kuvunwa siku 90 mpaka 150 tangu kupanda mbegu kutegemeana na aina. Vitunguu
vinavunwa kwa mikono. Mimea inang’olewa au kuchimbuliwa kwa kutumia rato (jembe
uma). Baada ya kuvuna vitunguu vinaweza kuachwa shambani vikiwa vimefunikwa na majani
kukinga jua kali kwa muda wa siku mbili au tatu kutegemeana na hali ya hewa.
Lengo ni kuimarisha ngozi ya vitunguu na kufanya michubuko na majeraha madogo
madogo yanayotokea wakati wa kuvuna kuwa magumu na kutengeneza mokovu ambayo
yanazuia vimelea vya magonjwa kuingia ndani. Pia kupunguza unyevu kwenye majani
na mashina na kuruhusu sehemu ya chini ya shingo kufunga. Ikiwa usalama ni mdogo,
vitunguu vinachambuliwa na kukatwa majani na mizizi na kuanikwa sehemu
nyingine.
|
Vitunguu vilivyong'olewa |
3.2 KUCHAMBUA
· Tenga vitunguu
vilivyooza, kuchubuka na kupasuka. Vitunguu vizuri vikaushwe peke yake.
· Iwapo vitunguu
vitahifadhiwa kwa kuninginiza kwenye chaga, basi shingo zisikatwe, bali zisukwe
na kufungwa pamoja, na kuninginizwa.
|
Watu wakichambua vitunguu |
3.3 KUKAUSHA
Hatua hii ni
muhimu ili kupunguza unyevu, kufanya vitunguu viwe vigumu na kuwa katika hali ya
kulala bwete.Vitunguu vinaweza kukaushwa kwa kuninginiza kwenye chaga
zilizopangwa mfano wa dari ndani ya banda au kutandaza kwenye kichanja chenye
kuruhusu mzunguko wa hewa pande zote, chini ya kivuli sehemu kavu. Epuka
kukausha vitunguu chini kwenye aridhini na hasa sehemu zenye jua kali. Jua linababusha
vitunguu na kusababisha uharibifu. Ukaushaji huchukua muda wa siku 7 au zaidi
kutegemeana na hali ya hewa.
3.4 KUPANGA
MADARAJA
Vitunguu
vinachambuliwa tena baada ya kukausha ili kuondoa vitunguu vyote vyenye ugonjwa
au dalili za ugonjwa, vilivyoota na kutoa mizizi na vyenye shingo nene.
Vitunguu vinapangwa kwenye madaraja mbalimbali kufuata ukubwa, umbo au rangi.
Hii inawezesha kuapta soko zuri na kuepukana na upotevu mkubwa wakati wa kuhifadhi.
3.5 KUFUNGASHA
NA KUWEKA VITAMBULISHO
|
Mfano wa kifungashio |
Vifungashio
vinavyopatikana ni mifuko ya nyavu vyenye uwezo wa ujazo wa kilo 20 au magunia
ya katani. Mifuko ya nyavu ina ujazo mdogo na pia inarahisisha ubebaji. Magunia
ya katani yanatumika lakini yanaficha vitunguu visionekane pia vinachukua mzigo
mzito na kuleta usumbufu wakati wa kupakia na kupakua. Vitambulisho vinawekwa
kwenye vifungashio ili kusaidia wasafirishaji kujua mzigo ulikotoka na pia
kutangaza bidhaa inayohusika kwenye masoko ya nje na ndani.
Kwa soko la nje vitambulisho
vinatakiwa na habari zifuatazo:
|
Mfano wa lebo kwenye paketi ya vitunguu |
· Jina la bidhaa
mf. Vitunguu Mango’la Red
· Uzito kamili
mf. 20 kg
· Jina na anwani
ya mkulima au kikundi, jina na anwani ya msafirishaji
· Jina la kijiji
wilaya, Mkoa na nchi mf. Igurusi, Mbarali, Mbeya, Tanzania
· Grade 1
Kwa soko la
ndani vitambulisho vinakuwa na habari zifuatazo:
· Jina la
bidhaa.mf.vitunguu Mango,la Red
· Uzito kamili
mf. 20 kg
· Jina la
mkulima au kikundi na anwani John Geda au Jitegemee, Box 200, Mbarali Mbeya
· Jina na anwani
ya msambazaji mf: Mr. Saidi Mbaga Box 670, Mbeya
|
Vitunguu vilivyowekwa kwenye magunia |
3.6
KUSAFIRISHAJI
Uangalifu wakati
wa kupakia, kusafirisha na kupakua ni muhimu ili kuepukana na uharibifu na upotevu
wa vitunguu. Mara nyingi vitunguu vinaharibika kutokana na ujazo kupita kiasi
kwenye vifungashio na vyombo vya usafiri, pia kutokana na upakiaji na mpangilio
mbaya, ambao unasababisha ugandamizaji na kubonyea kwa vitunguu.
|
Vitunguu vikisafirishwa |
Wakati wa
usafirishaji yafuatayo yazingatiwe:-
· Kutumia vyombo
vya usafiri vinavyofaa hasa magari yenye nafasi ya kutosha na yenye kupitisha
hewa
· Kupanga mifuko
katika tabaka zenye safu zisizodi tatu
· Mifuko
isitupwe wakati wa kupakia na kupakua
· Vitunguu
visichanganywe na mazao mengine.
3.7 KUHIFADHI
Vitunguu
vinahifadhiwa kwenye maghala bora kama kribu au mabanda ambayo yanaruhusu hewa
na paa kuezekwa kwa manyasi ili kupunguza joto.
|
Vitunguu kwenye kribu |
Hifadhi kwenye kribu
Kribu inajengwa
kwa fito au mianzi na kuinuliwa juu mita moja toka usawa wa aridhi. Upana wa
kribu uwe kati ya sm 60 na 150 ili kuruhusu upepo kupita kwa urahisi. Upepo
unaondoa unyevu na joto kwenye vitunguu. Kribu igawanywe sehemu mbili zenye
kina cha sm 60 kila moja na kutenganishwa na uwazi was m 30, ili kuruhusu
mzunguko wa hewa.
Wakati wa kutengeneza
kribu yaafutayo yazingatiwe:-
· Kribu ijengwe
kwenye sehemu yenye upepo
· Kribu iezekwe
kwa nyasi ili kudhibiti joto na jua
· Miguu ya kribi
iwekwe vizuizi vya panya.
· Weka vutunguu
tabaka mbili na kina cha vitunguu kisizidi sm 60
Hifadhi kwa
kuninginiza vitunguu kwenye banda
Hili ni banda
lenye uwazi mkubwa, lenye upana usiozidi mita tano, na urefu toka chini hadi juu
usizidi mita 2½. Banda linajengwa kwa miti, fito, mbao au mianzi na vitunguu vinahifadhiwa
kwa kuninginiza kwenye fremu za fito ndani ya banda. Safu za vitunguu hupangwa
kufuata urefu wa banda na kimo cha banda. Urefu wa banda huelekezw a kwenye mkondo
wa upepo ili kuruhusu upepo kuingia na kutoka. Banda liezekwe kwa nyasi ili kudhibiti
joto na jua. Kribu au banda vinahifadhi vitunguu vizuri kwa muda wa miezi sita
bila kuharibika.
|
vitunguu vilivyoning'inizwa |
3. 8. UPOTEVU WA
VITUNGUU GHALANI
Vitunguu vingi
hupotea wakati wa kuhifadhi kwa sababu ya:-
· Kuoza
· Kuota (toa
majani na mizizi)
· Kupoteza uzito
3.8.1. KUOZA
Kuoza kwa
vitunguu vikiwa ghalani kunasababishwa na vimeliea vya fangasi au bacteia. Joto
pamoja na unyevunyevu ndani ya ghala, kunasababisha kuzaliana na kuongezeka kwa
vimelea vya magonjwa
Kudhibiti:
· Weka ghala
katika hali ya usafi, kausha vizuri na chambua vitunguu ili kabla ya kuhifadhi.
a) Muozo Kitako
(Bottom rot or basal rot)
Vimelea vya aina
ya fungus vinavyoishi kwenye udongo, vinashambulia sehemu ya chini ya vitunguu.
Vimelea vinapenya kwenye sehemu zenye michubuko, inayotokea wakati wa palizi, kuvuna
au kusafirishwa. Vitunguu vinaoza na baadaye vinakauka na kusinyaa.
Njia zifuatazo zinadhibiti:-
· Mzunguko wa
mazao
· Kuchambuaji
mzuri kabla ya kuhifadhi
· Kuepuka
michubuko wakati wa palizi na kuvuna
b) Ukungu mweusi
(Black mould)
Ugonjwa huu
unaletwa na vimelea vya fangasi, vinavyoishi kwenye udongo. Vimelea vinazaliana
katikati ya maganda na ukungu mweusi kama poda unaonekana. Baadaye maganda yanasinyaa
na kuvunjika.
Kudhibiti
· Kutumia
mzunguko wa mazao
· Kukagua ghala
mara kwa mara na kuondoa vitunguu vilivyooza
· Kuweka ghala
katika hali ya usafi.
· Kuondoa
masalia ya vitunguu na kuchoma moto.
c) Kuoza shingo
(Neck rot)
Vimelea vya
fangasi vinashambulia vitunguu vikiwa shambani kabla ya kuvuna. Ugonjwa hauonekani
mpaka vitunguu vikomae, vivunwe, vikaushwe na kuhifadhiwa ghalani, ndipo ugonjwa
hujitokeza. Ugonjwa unasababisha kuoza kwa vitunguu. Maganda ya vitunguu yanalainika
kuanzia shingoni na nyama ya kitunguu huwa na sura ya maji maji. Vitunguu vilivyooza
vinyauka na kusinyaa.
Kudhibiti;
· Kukausha
vitunguu vizuri kabla ya kuhifadhi
· Kuchoma na
kuharibu masalia ya vitunguu shambani na ghalani.
d) Muozo laini
(Bacterial soft rot)
Ugonjwa
unasababishwa na vimelea vya bacteria. Dalili kubwa ya ugonjwa huu ni kulainika
kwa vitunguu na kutoa harufu mbaya. Ukiminya kitunguu maji yenye harufu mbaya
yanatoka kwenye shingo. Muozo laini unatokea wakati hali ya hewa ikiwa na unyevunyevu
na jotoi. Pia vitunguu vyenye shingo nene ambavyo havijakauka vizuri ni sehemu
nzuri sana ya vimelea kuzaliana.
Kudhibiti:
· Ukaushaji wa
haraka na wa uhakika baada ya kuvuna unapunguza sana ugonjwa huu
3.8.2 Kuota na
kupoteza uzito wa vitunguu
Vitunguu
vinakuwa katika hali ya kulala bwete bila kuota kwa zaidi ya miezi sita ikiwa
hali ya hewa ghalani ni nzuri. Unyevunyevu mwingi ghalani ni adui mkubwa wa
vitunguu vilivyohifadhiwa kwani inasababisha kuota kwa majani na mizizi. Pia
hewa ikiwa kavu sana vitunguu hupoteza maji upesi na kusinyaa. Kuongezaka kwa
joto na unyevunyevu ndani ya ghala kutokana na mzunguko mbaya wa hewa, uchafu
ghalani, ukaushaji na uchambuaji mbaya vinasababisha uharibifu kubwa wa
vitunguu ghalani
Kudhibiti ;
· Ghala liwe
safi pia liwe na uwezo wa kupitisha hewa kavu na ubaridi wa kutosha.
· Ghala lijengwe
sehemu yenye upepo na kuruhusu mzunguko mzuri wa hewa.
· Vifungashio
vya vitunguu vipangwe vizuri ili kuruhusu hewa kupita juu na chini.
· Vitunguu ndani
ya kribu/ghala vijazwe kina cha sentimeta 30-50.
· Vitunguu
vichambuliwe vizuri kabla ya kuhifadhi.
· Vitunguu
ghalani vikaguliwe mara kwa mara ili kuondoa vitunguu vilivyoharibika
4.0 SOKO LA
VITUNGUU
Kutokana
na uhitaji wa matumizi ya kila siku ya zao hili la vitunguu, uhitaji wake umekuwa
mkubwa siku kwa siku. Wapo watu walioweza ona fursa hii na kuamua kuifanyia kazi.
Kutokana na uhitaji wake kuwa mkubwa inchini kwetu,ni vyema tukaweza jua bei
yake ili kumwezesha mtu kutambua uhalisia wake.
Bei
ya kuuzia vitunguu shambani wakati was msimu wa vitunguu na endapo vimelimwa
kwa wingi basi bei ya gunia inakuwa kati ya shilingi za kitanzania 60,000/=
mpaka 80000/=. Inapokuwa sio wakati wa msimu na walimaji wamekuwa wachache na sokoni
uhitaji unakuwa ni mkubwa basi bei yake ni kati ya shilling za kitanzania 150,000/=
mpaka 200,000/=. Bei za sadolini kwa
sehemu zilizombali na soko ni kati ya shilingi za kitanzania 7,500/= mpaka 8,000/=.
Bei ya kilo moja kwa sehemu zilizombali na soko ni kati ya shilingi 2800/= mpaka
3500/=, (hata hivyo bei zinabadlika kulingangana sehemu husika).
|
Vitunguu vinavyooza |
4.1 UUZAJI WA
VITUNGUU
Watu wa aina
mabalimabali wanahusika na ununuzi na uuzaji wa vitunguu wakiwa ni pamoja na: wakulima,
wachuuzi, wafanya biashara ndogondogo, wauza jumla, wauza rejareja,
wasafirishaji na madalali.
Ili koboresha
uuzaji na kipato ni muhimu kuzingatia yafuatayo:
· Kuboresha
ujazo kwa kufuata vipimo vinavyokubalika (kufuta lumbesa)
· Kupeana habari
za masoko na bei.
· Kuboresha
usafirishaji kwa kutumia vikundi.
· Kuwepo na
mtiririko wa kuuza vitungu mwaka mzima, kwa kuboresha hifadhi ikiwa ni pamoja
na maghala.
· Kutathimini na
kuzingatia ubora wa vitunguu.
· Kutathimini na
kuboresha ufungashaji na usafirishaji
HITIMISHO
Tunatambua
ya kwamba zao hili linafaida kuanzia shambani mpaka mtumiaji wa mwisho. Sasa ni
vyema kabla ya kuanza kilimo hichi kuhakikisha umetatua maswala yafuatayo:
i.
Eneo
(kununua au kukodi),
ii.
Maji
(kilimo cha umwagiliaji au kutegema mvua),
iii.
Nguvu
kazi kwa ajili ya maandalizi ya shamba
iv.
Msimamizi
(Kujua kama utasimamia wewe mwenyewe au utamwajiri mtu kwa kazi hiyo)
v. Gharama(gharama za maandalizi,upandaji,ukuzaji, na utafutaji wa masoko na
uuzaji)
Ninaimani
ukizingatia haya itakusaidia kujua uanze na mradi wa ukubwa gani. Pia kwa
maelezo haya machache itakusaidia kupata mwanga zaidi juu ya fursa hii na endapo
utahitaji kuuanza utajua ni wapi pa kuelekea ili kupata maelezo sahihi ya kiutaalamu. acha comment yako hapa chini ikiwa unachochote cha kusema
Labels: KILIMO BORA, MAZAO YA VIUNGO, VITUNGUU