Mihogo inaweza kuanza kuvunwa baada ya miezi 9 – 12 tangu kupandwa. Inashauriwa kuvuna katika katika kipindi cha jua kwani wakati wa mvua kiwango cha wanga kwenye muhogo hupungua.
Ndugu msomaji habari yako na karibu tena katika muendelezo wa mafunzo yetu ya kilimo bora. Wiki iliyopita, Jumatatu (kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wetu) tulishindwa kukulete makala kama ilivyo kawaida yetu, nichukue fursa hii kukuomba radhi kwa usumbufu ulioupata.
Leo nimekuandalia makala hii ya kilimo cha muhogo. Kutokana na sifa yake ya kuvumilia ukame kipindi hiki ni muafaka kabisa kwa maandalizi na upembuzi juu ya kilimo cha mihogo kwa msimu ujao wa mvua za vuli. Natumai katika makala hii utajifunza mambo yote muhimu unayohitaji kujua kuhusu muhogo. Karibu...
|
Majani ya muhogo - hutumika kama kisamvu (Mboga) |
Utangulizi
Zao la muhogo ni muhimu sana kwa Tanzania, zaidi kwa wakulima wadogo wenye kipato cha chini. Wakulima wengi huchanganya zao la muhogo na mazao mengine kama vile kunde, mbaazi, njugumawe, n.k. Umuhimu wa zao hili ni kutupatia chakula na wakati mwingine kwa biashara. Kwa kanda ya kusini muhogo ni chakula kikuu ambacho kinachuku asilimia 75 ya chakula kwa maeneo yote ya mikoa ya Lindi na Mtwara.
Kwa siku za karibuni, muhogo unaongoza kwa kuongezeka katika umaarufu kuliko mazao yote ya chakula nchini. Watalaam wanazungumzia umaarufu wa muhogo kuwa ni (pamoja na mambo mengine) uwezo wake wa kustahamili hali ya hewa mbaya kama ukame na mvua zisizoaminika, kutoa mazao mengi kwa eneo na kustahamili mashambulizi ya magonjwa na wadudu.
Hata hivyo uzalishaji wa muhogo kwa eneo bado ni wa viwango vya chini mno. Zipo sababu nyingi zinazo sababisha kuwepo kwa hali hii kama vile:
- Ukosefu wa mbegu bora za mihogo za kutosha
- Wakulima kuendelea kungangania mbegu zao za asili kuliko mbegu bora licha ya uzalishaji mdogo na kushambuliwa na magonjwa na wadudu.
- Ukosefu wa masoko ya kuaminika ambayo yangeshawishi wakulima kulima mbegu za kisasa ambazo zimeandaliwa kibiashara.
- Wakulima wengi kutotumia teknolojia sahihi za usindikaji ambazo ni mbinu mbadala za hifadhi za asili.
Kwa muda mrefu tatizo kubwa la zao la muhogo ni ukosefu wa teknolojia ambazo zina uwezo wa kuongeza thamani wa muhogo kama chakula chenye ubora kwa familia za mijini na vijijini. Vikundi mbalimbali vya uzalishaji na usindikaji vimeundwa na muhogo umeanza kuthaminwa kwani unga wake unatumika kutengenezea vyakula kama maandazi, chapati, chichili, keki na vingenevyo vingi. Ugali wa muhogo umeongezeka thamani kutokana na ubora wa unga uliosindikwa kwa kwa teknolojia ya kisasa.
Madhumuni ya Mogriculture Tz kutoa makala hii ni kutoa maelekezo juu kilimo bora cha zao la muhogo ili kusaidia wakulima kuinua viwango vya ubora na wingi wa mazao hivyo kujihakikishia usalama wa chakula na kujiongezea kipato.
Umuhimu na Matumizi ya Muhogo
- Muhogo ama (kitaalam) manihot esculentum, ni muhimu sana kwa Tanzania kutokana na sifa zake za kuvumilia ukame, kustawi kwenye maeneo yenye rutuba kidogo hivyo kuhitaji gharama ndogo za uzalishaji. Kwa hali hiyo, zao hili hulimwa sana na wakulima wadogo walio wengi wenye kipato kidogo.
- Kwa wakazi wa vijijini, muhogo huvunwa, kutolewa ganda la juu na kuanikwa hadi kukauka maarufu kama makopa. Kwa kawaida makopa hutwangwa kwenye kinu na kupata unga ambao hutumika kama uji au ugali. Makopa mara nyingi hutunwa ama kuhifadhiwa kwenye dari ya nyumba ambako hufukiziwa moshi wa moto ili yasipukuswe.
- Kutokana na hali hiyo, wakulima wengi hulima muhogo mchungu ambao haupukuswi kwa urahisi. Kwa vile muhogo mchungu una sumu nyingi aina ya cyanide, hufanya kiasi kidogo cha muhogo kiliwe kwa kutafuna ukiwa mbichi ama kupikwa kama futari.
- Kwa wakazi wa mijini, sehemu kubwa ya mihogo hutumika kama futari au kitafunwa kwa chai ama humenywa na kukaangwa kama chips maarufu kama chips dume.
- Kutokana na kuongezeka kwa teknolojia za usindikaji, unga wa muhogo hutumika kutengenezea biskuti, chapati,maandazi,chichili,keki na vyakula vingine vingi vinavyotengenezwa kwa kutumia unga wa ngano.
|
Chakula kilichotengenezwa kwa muhogo |
Mazingira na Aina za Mihogo
Mazingira yanayofaa
Muhogo ni zao la jamii ya mizizi. Hustawi vizuri katika maeneo yaliyopo kwenye mwinuko wa mita 0 hadi 1500 toka usawa wa bahari. Zao hili hustawi vizuri kwenye maeneo yanayopata mvua ya wastani wa milimita 750 mpaka milimita 1200 kwa mwaka.
Muhogo hupendelea udongo wa kichanga usiotuamisha maji. Udongo wa kichanga husaidia mizizi kupenya kwa urahisi na kupevuka. Vile vile muhogo una sifa ya kuvumilia hali ya ukame wa muda mrefu.
Aina za Mihogo
Kuna zaidi ya aina 45 za mihogo zinajulikana nchini Tanzania. Zaidi ya asilimia 80 ya mihogo ni ya asili. Hivyo ni kusema wakulima wengi hawatumii mbegu bora. Ingawa wakulima wengi pia hupendelea kulima mihogo michungu kwa sababu haishambuliwi sana na wadudu ama magonjwa shambani na makopa yake yanahifadhika kwa urahisi, zaidi ya asilimia 70 ya mihogo ni mihogo baridi. Bofya hapa kujua mbegu bora mpya za mazao ili uweze kuachana na matumizi ya mbegu za asili.
Mihogo ya asili
Mihogo ya asili ni ile iliyoendelea kulimwa miaka mingi iliyopita na kurithiwa vizazi kwa vizazi. Mihogo hii ina sifa za jumla zifuatazo:
- Hutoa mavuno wastani wa tani kwa Hekta.
- Mingi inachukua muda mrefu kukomaa
- Inahifadhika shambani kwa muda mrefu bila kuoza
- Hushambuliwa na magonjwa kama Ugonjwa wa michirizi ya ki-kahawia, batobato na blaiti.
- Hushambuliwa na wadudu milibagi
- Imezoeleka na wakulima hivyo wanaijua tabia yake na jinsi ya kuitunza.
Mihogo Bora
Hii ni mihogo iliyofanyiwa utafiti wa pamoja baina ya watalaam na wakulima na kuthibitishwa na Kamati ya Mbegu ya Taifa kama inafaa. Kituo cha Utafiti wa Mazao ya Kilimo cha Naliendele, Mtwara kimebaini mbegu bora aina ya Naliendele na Kiroba ambazo zina sifa zifuatazo:
- Hutoa mavuno ya tani 19 hadi 30 kwa Hekta.
- Hustahamili mashambulizi ya ugonjwa Michirizi ya kikahawia, batobato na blaiti.
- Hukomaa miezi tisa tu baada ya kupanda.
Kuandaa shamba
Inashauriwa kuandaa shamba mapema kabla ya msimu wa mvua haujaanza. Zifuatazo ni hatua za msingi katika kuandaa shamba:
- Kufyeka msitu au vichaka
- Kung’oa na kuchoma moto visiki
- kulima na kutengeneza matuta.
Uchaguzi wa mbegu bora za kupanda
Aina bora za mbegu za muhogo
Mpaka sasa hivi kuna aina mbili za mbegu bora ambazo zimethibitishwa kwa wakulima. Mbegu hizi huvumilia magonjwa (batobato na matekenya), pia huzaa sana ukilinganisha na mbegu za kienyeji.
Huzaa tani 19 kwa hekta moja, na inaweza kuvunwa kuanzia miezi 9 toka ipandwe.
Huzaa tani 25 – 30 kwa hekta moja, na inaweza kuvunwa kuanzia miezi 9 toka ipandwe.
Katika kuchagua mbegu inayofaa, pamoja na mambo mengine, zingatia yafuatayo:
- Mbegu itokane na shina lililokomaa vizuri
- Isitokane na shina la muhogo ulioshambuliwa na magonjwa.
- Macho yake yasiwe yamekaribiana sana au kuachana sana
Upandaji wa Muhogo
Muda wa kupanda
Kanda ya ziwa: December mpaka January mwishoni
Nyanda za juu Kusini: November mwanzoni na
Kanda ya Mashariki: kuanzia October mpaka December
Urefu wa kipande cha shina cha kupanda: Baada ya kuchagua mbegu hatua inayofuata ni kukata shina lako la muhogo katika pingili ndogo ndogo tayari kwa kupanda. Inapendekezwa pingili ziwe na urefu wa sentimita 30. Hata hivyo, urefu wa pingili utategemea sana idadi ya macho yaliyopo kwenye hicho kipande. Inapendekezwa kipande kimoja kiwe na macho manne hadi sita.
Nafasi ya kupanda: Nafasi ya kupanda kwa shamba linalokusudiwa liwe na muhogo mtupu ni mita moja toka shina hadi shina na mita moja kati ya mistari. Kwa shamba ambalo mkulima anakusudia kuchanganya mazao, inashauriwa nafasi ya kupanda iwe mita 2 hadi mita 4 (kwa kutegemea aina ya mazao yanayochanganywa) kati ya mistari na mita moja toka shina hadi shina.
Kuna njia tatu za upandaji wa muhogo:
- Kulaza ardhini (Horizontal)
- Kusimamisha wima (Vertical) na
- Kuinamisha ( Inclined/Slunted)
|
Shamba la mihogo |
Palizi
Katika miezi minne ya mwanzo muhogo unahitaji kupata chakula cha kutosha na mahitaji mengine ya msingi ili uweze kukua na kujenga mizizi mikubwa na imara. Hivyo inashauriwa kufanya palizi la kwanza mapema, angalau mwezi mmoja baada ya kupanda ili kuepukana na magugu yanayochipua haraka baada ya mvua za mwanzo kunyesha.
Kwa kawaida palizi hufanywa kwa kutumia jembe la mkono au dawa ya kuulia magugu. Njia nyingine ya kudhibiti magugu ni kupanda mimea yenye majani yanayotanda juu ya udongo. Palizi kwa kawaida hufanywa kila inapoonekana kwamba magugu yameota kiasi cha kuathiri ustawi wa muhogo, hivyo unaweza kupalilia mara 3 au 4 zaidi baada ya palizi ya kwanza hadi muhogo kukomaa.
Kuchanganya mazao
Utafiti unaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 80 ya mashamba ya muhogo Tanzania yanachanganywa na mazao mengine. Sababu kubwa zinazotolewa kuhusiana na hali ni kwamba wakulima wanafaidika kwa kupata mavuno ya ziada kama kunde, karanga mahindi maharage, korosho ama njugu.
Kwa kuchanganya mazao, mkulimalicha ya kuimarisha uhakika na usalama wa chakula, anaweza kuuza mazao mchanganyiko na kujiongezea kipato. Vile vile mazao ya jamii ya mikunde yanasaidia kuongeza rutuba ya udongo.
Hata hivyo, mazao mchanganyiko ni budi yasilete ushindani na muhogo katika kujipatia chakula, hewa, mwanga, unyevu na mahitaji mengine ya mmea yanayoweza kuathiri ustawi wa muhogo. Inashauriwa pia kuzingatia muda wa kupanda, yaani muhogo upandwe mvua za kwanza ili mazao mchanganyiko yasiweze kuzidi na kuutawala muhogo.
Uvunaji
Mihogo inaweza kuanza kuvunwa baada ya miezi 9 – 12 tangu kupandwa. Inashauriwa kuvuna katika katika kipindi cha jua; kwani wakati wa mvua kiwango cha wanga kwenye muhogo hupungua. Mihogo hutoa mavuno ya tani 19 hadi 30 kwa hekta kutegemeana na aina ya mbegu (variety).
|
Mihogo baada ya kuchimbuliwa |
Usindikaji bora
Usindikaji bora wa muhogo unafanyika kwa sababu kuu tatu:
- Kurahisisha/kuharakisha ukaushaji
- Kuondoa sumu (cyanide) ilyoko kwenye baadhi ya aina za mihogo
- Kuongeza ubora wa unga utokanao muhogo wenyewe.
Njia bora za usindikaji
- Kwa kutumia mashine aina ya Grater
Hii hutoa chembechembe laini za muhogo, ambazo baadae hukamuliwa kwa kutumia kifaa kingine kiitwacho “presser” ili kuondo sumu iliyoko kwenye muhogo. Mashine hii hutumika hususani kwa muhogo mchungu.
- Kwa kutumia mashine aina ya chipper
Mashine hii hutoa vipande vidogo vidogo (chips). Mashine hii hutumika hasa hasa kwa ajili ya mihogo mitamu/baridi.
Matumizi ya Muhogo
- Muhogo unaweza kupikwa wenyewe kama chakula au kutengeneza unga
- Unga wa muhogo unaweza kutengeneza vitu vyotekama vinavyotengenezwa na unga wa ngano kama vile biskuti, chapatti, maandazi, chichili, keki n.k.
- Pia muhogo huweza kutumika viwandani kutengeneza bidhaa nyingine kama vile wanga.
Magonjwa na Wadudu Waharibifu wa Muhogo
Magonjwa
Kuna magonjwa mawili ambayo ni muhimu sana na yanapunguza uzalishaji wa zao la muhogo.
a) Ugonjwa wa Matekenya au Ugonjwa wa michirizi ya kahawia katika muhogo
Ugonjwa huu ni maarufu kwenye sehemu zenye miinuko iliyo na urefu chini ya mita 300 na unapatikana kidogo sana kwenye miinuko ya mita 500 na kuendelea ambako uenezaji wake wa kawaida hautokei kabisa.
Visababishi
Matokeo ya uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba ugonjwa huu ulienezwa na mdudu mweuupe au inzi mweupe (whitefly) mwenye mabawa madogo.
Dalili za Ugonjwa
Sehemui zote za muhogo zinaweza kuonyesha dalili za uambukizo wa ugonjwa huu lakini ni vipengele gani vya ugonjwa na ni kwa kiwango gani hutegemea hali ya mzingira, hatua ya kukua kwa mmea kwa kulinganisha.
Dalili ya kwanza: Chlorosis rangi ya njani hutokea kwanza pembezoni mwa vena ndogo baadae huathtiri vena ndogo zaidi na inaweza kuwa doa (chlorosis) la rangi ya njano.
Dalili ya pili: Rangi ya njano ambayo haihusishwi vizuri na vena isipokuwa katika mbaka ya mviringo kati ya vena kuu kwenye hatua za mwisho za ugonjwa sehemu kubwa ya lamin inaweza isiathirike, majni yenye ugonjwa hubaki yameshikilia kwenye mmea kwa muda wa wiki kadhaa.
Huonekana kwenye tisu ya shina changa la kijani, jeraha la zambarau au kahawia linweza kuoneakan nje na kuingia ndani hadi kwenye gamba baaada ya kubandua gome la nje. Pia jeraha la nekrotiki kwenye kovu la shina hutokea baada ya majni kudondoka kutokana na umri wa mmea. Tawi/shina hufa kuanzia kwenye nch kuelekea chini na kusababisha kufa kwa mmea wote.
Kwa kawaida hutokea baada ya dalili za majani na wakati wa kipindi kati ya uambukizo na kufa, amabpo kifo cha mizizi hutokea kuanzia miezi 5 toka kupandwa. Dalili za mizizi zinabadilika nje ya mizizi na zinaweza kuwa kama kizuizimwanga au shimo au kufa kwenye gome.
Tishu inayo zunguka mshins ina doa la rangi ya kahawia au nyeusi. Wakati mwingine mizizi huonekana kuwa yenye afya kwa nje bila kuwa na matatizo yaliyowazi au bila kupungua ukubwa, lakini ikikatwa huonekana kufainakufa au rangi ya njano.
Uambukizaji na ueneaji
Ugonjwa wa CBSD unaambukizwa kwa njia ya vipandikizi vinavyotokea kwenye mimea iliyoathiriwa vinavyosababisha mmea kuonesha kwenye majani dalili za ugonjwa. Kwa kuwa muhogo kwa kawaida huzalishwa kwa njia ya vipandikizi ugonjwa huu huingizwa kwenye sehemu mpya zilizopandwa kwa kutumia vipandikizi vilivyoambukizwa.
Kwa aina zinazovumilia sana kwenye hali za mabondeni, dalili mbaya sana hutokea wakati ugonjwa ukigundulika katika hatua za mwanzo. Uchunguzi umeonesha kwamba Bemisia afer ni mdudu/kisababishi ambacho ndicho kinachohusiana na maendeleo ya hivi karibuni kuhusu uhamishaji wa visababishi kama “ipomovirus”. Mara nyingine inaonesha wadudu weupe (White flies) na kutokana na hali hiyo bado uchunguzi unaendelea zaidi.
Udhibiti/Kuzuia
- Njia ya msingi ya kuzuia/kudhibiti ugonjwa wa CBSD ni kuchagua mbegu kutoka kwenye mimea isiyo na dalili ya ugonjwa.
- Ubora wa mashina unahitaji kutunzwa kwa kuendelea kuchagua na kuangamiza ile iliyoambukizwa ambayo inaonekana wakati wa kuchipua.
- Hakikisha kuwa unapanda mbegu bora za muhogo ambazo zinastahimili maambukizi ya magonjwa.
- Hakikisha kuwa wakati wa uvunaji uonapo hali ya kuoza kwa mizizi ya mhogo ichome moto ili kutokomeza ugonjwa huo.
- Kuelewa dalili za ugonjwa wa CBSD kwa ajili ya kuchukua tahadhari ya kutokomeza ugonjwa huu.
- Hakikisha kuwa unaendelea kutunza mbegu bora zinazoonekana kuvumilia magonjwa sana.
- Hakikisha kuwa shamba la mhogo linakuwa safi kwa ajili ya kupunguza visababishi vya ugonjwa wa CBSD
b) Ugonjwa wa batobato au ukoma wa majani (Cassava Mosaic Disease - CMD)
Ni ugonjwa ambao ulienezwa kwa mara ya kwanza hapa Tanzani mwaka 1894, na baadae uliripotiwa katika nchi nyingine nyingi za Afrika Mashriki, Afrika Magharibi na Afrika ya Kati na sasa unafahamika kuwa upo maeneo yote yanayolimwa muhogo Afrika. Katika viwango vya kuwepo kwa ugonjwa wa CMD na katika uwingi wa hasara zinazopatikana kutokana na CMD ni kati ya 15 – 20%. Hii ni sawa na tani milioni 15 – 18 zikilinganishwa na makadirio ya shirika la kilimo na chakula duniani ya tani milioni 85 ya mwaka 1997.
Visababishi
Tangu ugonjwa wa CMD ulipoenezwa kwa mara ya kwanza, visababishi vilichukuliwa kuwa ni virusi kwa sababu ya kukosekana kisababishi kingine. Kwa hiyo kutokana na kuwa mtazamo huu unalingana na matokeo ya uchunguzi wa awali inaonesha kwamba ugonjwa huu huenezwa na mdudu nzi mweupe (white fly).
Pia uchunguzi wa mara kwa mara umesababisha utambuzi wa virusi vya aina mbalimbali na tofauti kama ifuatavyo:
- Ugonjwa wa batobato unaosababishwa na virusi vya Africa cassava mosaic virus
- Ugonjwa wa batobato unaosababishwa na virusi vya Afrika mashariki (East Africa cassava mosaic virus)
- Ugonjwa wa batobato unaosababishwa na virusi vya India (Indian cassava mosaic virus)
Dalili za ugonjwa wa batobato (Cassava Mosaic Disease - CMD)
- Dalili hutokea kwenye jani lenye ruwaraza za michirizi ambazo huathiri sehemu zisizokunjamana za kutolea hewa na hufahamika katika hatua za awali za ukuaji wa jani.
- Sehemu za kloritiki hushindwa kutanuka hadi mwisho, hivyo mvutano unajitokeza kutokana na ukuaji usiolingana na jani au majani madogo yaliyoharibika.
- Majani yaliyoathirika sana hupungua ukubwa wa umbo, na hujikunja na kujitenga kwa sehemu zenye rangi ya njano na zenye rangi ya kawaida ya kijani.
- Mmea hudumaa na majani machanga hupatwa na uvimbe.
- Kloritiki ya jani inaweza kuwa ya rangi ya manjano nyepesi au rangi inayokaribia nyeupe yenye kijani kidogo au kupauka kuliko ilivyo kawaida.
Uambukizaji na uenezaji
- Ukoma wa mhogo huambukizwa kwenye vipandikizi vya shina ambavyo kwa kawaida hutumika kuzalishia mmea.
- Pia huenezwa na inzi mweupe (white fly) aitwae Bemisia tabaci G. Aina mbili za inzi au Mbu hao Bemisia (Preisner Hhosny na Aleorodius disperses R) pia huambukiza mihogo katika nchi za Afrika na India
- Usambazaji wa vipandikizi unaweza kusababisha kuenea kwa ugonjwa wa CMD katika maeneo mapya.
Udhibiti/kuzuia
- Hatua ya msingi ya kuzuia ugonjwa wa CMD ni kwa kuchagua vipandikizi kutoka kwa Mmea ambao hauna uambukizo wowote.
- Ubora wa mashina unahitajika kwa kuendelea kuchagua na kuangamiza kwa kung’oa ile Mihogo iliyoambukizwa ambayo inaonekana wakati wa kuchipua
- Hakikisha kuwa wakati wa kuvuna mihogo kwa ile iliyoathirika na ugonjwa wa CMD inaangamizwa kwa kuchomwa moto.
- Hakikisha kuwa unatunza shamba na kuwa safi ili kupunguza wadudu waenezao CMD.
- Hakikisha una elimu ya kutosha juu ya dalili za ugonjwa wa CMD>
Wadudu/Wanyama waharibifu
Wadudu hawa hushambulia kwenye ncha za mashina/matawi kwenye majani machanga. Athari zake ni kwamba majani ynadumaa na kujikusanya pamoja, hivyo basi kupunguza ukuaji wa mmea kwa ujumla. Vile vile urefu kati ya pingili na pingili huwa fupi sana.
- Cassava Green Mites (CGM)
Wadudu hawa hushambulia majani mapya sehemu za chini. Madhara yake sio makubwa.
Hawa ni weupe na hujishika kwenye shina na kufyonza maji kutoka kwenye mti wa muhogo. Vili vile wadudu hawa madhara yake sio muhimu.
Hawa hutafuna / hula mashina ya muhogo hasa wakati wa jua kali/kiangazi.
Hawa hushambulia muhogo ukiwa shambani kwa kuula, kama vile nguruwe, panya, wezi, n.k
|
Panzi pia hula majani ya mihogo |
Udhibiti/Kuzuia
Kwa upande wa wadudu wanaweza kudhibitiwa kwa njia zifuatazo:
- Kutumia dawa za kuulia wadudu
- Kutumia wadudu marafiki wa wakulima
- Kwa upande wa wanyama ni kuweka walinzi.
Ni matumaini yangu kuwa umejifunza mambo mengi mazuri kuhusu kilimo cha muhogo, sasa tumia angalau dakika mbili tu kutupatia mrejesho kwa kuandika comment yako hapa chini. Tukutane tena katika makala nyingine wiki ijayo, kazi njema.
Kabla hujaondoka; nimekuwekea makala hizi hapa muhimu nimeona zisikupite, bofya kuzisoma:
Labels: KILIMO BORA