Utangulizi
Jina la kitalaam ni Curcuma domestica au Curcuma longa na kwa kiingereza ni turmeric. Zao hili asili yake ni Mashariki ya Mbali, na linalimwa zaidi katika mkoa wa Tanga, Kagera, Kilimanjaro, Morogoro na Zanzibar. Binzari hutumika kwa mapishi ya nyama, samaki na
mapishi mengine kwa kuweka rangi yake ya njano. Hutumika zaidi na nchi za
mashariki kama India; nchi za Ulaya hutumia kidogo sana.
Soma: Fursa ya kilimo cha viungo Morogoro
Mahitaji na mambo muhimu katika uzalishaji
• Hali ya hewa
Humea vizuri maeneo yenye kiasi cha joto la nyuzi
24-26 za sentigredi na huzalishwa maeneo ya mwambao.
• Udongo
Udongo wenye rutuba na unaopitisha maji na usio na
mawe au changarawe. Mahitaji ya mvua ni milimita 1200-2000 kwa mwaka. Epuka
kusimama kwa maji shambani. Umwagiliaji unaweza kufanywa endapo maji
hayatoshelezi. Binzari inafanya vizuri ikipandwa sehemu ya uwazi. Ingawa pia
inaweza kuchanganywa na mazao mengine kama minazi.
• Uchaguzi wa mbegu
Mbegu zinazotumika hapa nchini ni za kienyeji bado.
Tunguu kubwa zenye ukubwa wa sm 2.5 hadi sm 3 hutumika kama mbegu. Kiasi cha
tani 1.7 za vipando huhitajika kwa hekta. Tunguu za kupandwa zisihifadhiwe kwa
zaidi ya mwezi mmoja kabla ya kupanda.
Soma Aina mpya za mbegu za mazao
• Nafasi ya upandaji
Nafasi
ya kupanda ni sm 15-25 kati ya mmea na mmea na sm 25-30 kati ya mstari na
mstari au sm 45-60 kati ya tuta na tuta.
• Mahitaji ya mbolea
Matumizi
ya mbolea hapa Tanzania si makubwa katika kilimo cha viungo. Tafiti zimeonesha
kuwa binzari hazioneshi kufanya vizuri kwenye mbolea za viwandani. Mbolea za
samadi zinaweza kutumika. Kiasi cha tani mbili hadi tatu za samadi kwa eka moja
kinatosha.
Soma mahitaji ya mbolea katika kilimo cha mahindi
|
Shamba la binzari |
Uvunaji
Uvunaji
hufanywa kwa kutumia majembe au uma. Binzari huvunwa wakati majani yamegeuka
rangi na kuwa njano au kahawia. Binzari isiyo na kambamba huvunwa kipindi cha
miezi sita toka kupandwa na miezi 18 hadi 21 kwa binzari iliyokomaa kutegemeana
na mahitaji ya soko.
Mavuno
ya tani 7 hupatikana endapo binzari ikipandwa peke yake. Mavuno hupungua kiasi
binzari ikipandwa mchanganyiko na mazao mengine kwa mfano mavuno ya tani 4.8
kwa hekta yatapatikana binzari ikipandwa na minazi.
Utayarishaji
Kabla
ya kuhifadhiwa binzari zichemshwe kwa dakika 45 hadi saa moja ili kuondoa
harufu yake ya udongo. Pia kuchemsha kunasaidia zikauke kwa pamoja. Binzari zichemshwe
mpaka kijiti kisicho na ncha kali kiweze
kutoboa kwa urahisi. Kisha ziepuliwe na
kuanikwa juani kawaida huchukua siku 10 hadi 15 ili zikauke kufikia kiasi
cha unyevu (moisture content) 5% hadi 10%. Binzari pia yaweza katwa vipande
vidogo vidogo ili kurahisisha kukauka. Baada ya hapo ziko tayari kutwangwa au
kusagwa kwenye mashine za kusagia viungo au kuhifadhiwa kama zilivyo.
Mashambulizi
ya wadudu na magonjwa
Tatizo
kubwa ni ugonjwa wa ukungu unaosababishwa na vimelea vinavyoitwa Colletotrichum
sp. na Glomerella cingulata. Dalili ni madoa ya kahawia kwenye majani
ambayo husambaa na kisha jani hukauka. Magonjwa haya yanaweza kudhibitiwa kwa
kupiga dawa za ukungu kama Dithane M-45 kila baada ya wiki mbili.
Masoko
Soko
la binzari linapatikana ndani na nje ya nchi.. Zao hili huuzwa katika nchi za
Uganda, Kenya, Uingereza, Ujerumani, Mashariki ya Kati, n.k. Binzari yaweza
kuuzwa ikiwa mbichi (mara tu baada ya kuvuna), ikiwa kavu au baada ya kusagwa
kulingana na mahitaji ya soko.
Ushauri: Wakulima
wanashauriwa kukausha binzari kwa uangalifu ili kutoharibu ubora wake.
Labels: KILIMO BORA, MAZAO YA VIUNGO