|
Milima ya Uluguru-Morogoro |
ASILIMIA 90 ya wananchi katika Halmashauri ya wilaya ya Morogoro ni
wakulima na wamekuwa wanakitumia kilimo kujiendeleza kiuchumi, wao na
halmashauri hiyo.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 halmashauri hiyo
inakadiriwa kuwa na watu 286,248. Kilimo cha mazao ya chakula na
biashara licha ya kuwanufaisha wakulima pia ni chanzo cha makusanyo ya
mapato katika
Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro. Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri hiyo, Yona Mark, anasema, ardhi katika halmashauri hiyo
imegawanyika kiuzalishaji kwa mazao ya chakula, matunda na kibiashara.
Anasema kwamba halmashauri hiyo ina ukubwa wa eneo la kilometa za
mraba 11,925.75 ambazo ni sawa na hekta 1,192,575 na kwamba, eneo
linalofaa kwa kilimo ni hekta 447,000. Mark anataja eneo linalotumika
kwa uzalishaji kwa kilimo na wakulima wadogo ni hekta 78,794.96 na jumla
ya mashamba 63 yana hati miliki. Anasema eneo linalofaa kwa kilimo cha
umwagiliaji ni hekta 28,075 , na kwamba hekta 100 zilizojengewa
miundombinu ya kuvuna maji na mvua.
Hekta hizo zimetengwa kwa wakulima wa vijiji viwili, Mlilingwa na
Matuli na wameanza kulima. Vijiji hivyo vyote vipo katika tarafa ya
Ngerengere, kila kimoja kimepatiwa hekta 50. Anasema, ukanda wa milima
unahusisha tarafa za Mkuyuni na Matombo na kwamba wananchi wa maeneo
hayo wanajihusisha na uzalishaji wa kilimo cha mahindi, muhogo,
migomba
na magimbi. Kwa mujibu wa Mark, wananchi hao pia wanalima machungwa,
mananasi, maembe, mashelisheli na mafenesi.
|
Mkoa wa Morogoro (Eneo lenye rangi nyekundu) |
Ukanda wa mabondeni unahusisha tarafa za
Mvuha, Bwakira, Mikese na
Ngerengere. Wananchi kwenye maeneo hayo wanalima mahindi, mpunga, mtama,
muhogo, migomba na magimbi. “Wilaya hii hutegemea kilimo kama njia kuu
ya kujipatia kipato, kilimo kwa kiwango kikubwa hutegemea mvua,“ anasema
Mark. Anasema, wananchi hao ni wazalishaji wa mazao mengine ya biashara
likiwemo la pamba, ufuta na alizeti. Pia mazao mengine yanayozalishwa
ni ya viungo ambayo ni
pilipili manga, mdalasini, tangawizi, karafuu,
hiliki, binzari na matunda.
Wakulima wa vijiji vya kata ya Kisemu, Tarafa ya Matombo, wanasifu
uwezeshaji wa serikali kwenye kilimo. Wanasema, uwezeshaji huo ni pamoja
na mafunzo ya kilimo bora, matumizi sahihi ya pembejeo hususani mbegu
na dawa za kuua wadudu waharibifu wa mazao . Uwezeshaji huo pia
unahusisha ujenzi wa masoko ya mazao katika baadhi ya vijiji vikiwemo
vya Mkuyuni na Mtamba. Masoko hayo yamekuwa chachu ya maendeleo ya
wakulima vijijini katika kuinua uchumi.
Mkulima katika kijiji cha Kisemu aliyejitambulisha kwa jina la
Francis Kobero, anasema wananchi wa tarafa ya Matombo wanategemea kilimo
cha mazao ya matunda , mboga , ndizi na mahindi kwa ajili ya kuwapatia
kipato cha kila siku. “Serikali imetujengea soko la kisasa hapa Mtamba,
kuwepo kwa soko hili, kumeongeza chachu ya biashara za kuuza mazao
yetu kwa bei nzuri kwa wafanyabiashara kutoka nje ya wilaya” anasema
Kobero.
Anasema soko limewasaidia kuuza mazao kwa bei nzuri na ziada ya faida
inatumika kufanya shughuli za kimaendeleo ukiwemo ujenzi wa nyumba
bora. “Mapato yanaweza kuongezeka kwa mkulima mmoja mmoja pamoja na ya
halmashauri pale wakulima watakapopatiwa elimu inayohusu uzalishaji
unaozingatia upatikanaji wa ongezeko lenye tija,” anasema mkulima huyo.
Mkulima wa mahindi na mpunga wa kijiji cha Mtamba, tarafa ya Matombo,
Agatha John anasema elimu ni tatizo kubwa kwa wakulima hivyo
kusababisha washindwe kupata mafanikio endelevu ya uzalishaji mazao
wenye tija. “Wakulima tukiwezeshwa kielimu ya matumizi bora ya mbegu na
mbolea tutaongeza uzalisha wa chakula na ziada itauzwa kwa ajili ya
kupata fedha za kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja, kijiji, kata hadi
taifa,” anasema.
Anasema ,
mazao ya viungo, hasa pilipili manga, mdalasini , hiliki,
karafuu na tangawizi yamekuwa na soko kubwa la nje ya wilaya hususani
Dar es Salaam na Zanzibar. “Kila mnada wa juma unapofanyika katika
masoko ya Mkuyuni, Mtamba na Mvuha , wafanyabiashara kutoka Dar es
Salaam na Zanzibar wanafika kununua mazao ya viungo katika masoko haya
na bei zake ni za juu,” anasema.
Mkulima Patric Mkude , anasema katika kipindi cha nyuma wakulima
walikuwa hawatumii mbolea , lakini kwa kuwa ardhi imekosa rutuba na
mavuno kupatikana kidogo , wameanza kuitumia ili kuzalisha mazao kwa
wingi yatakayowapatia kipato kikubwa. Wakulima wa tarafa ya Matombo,
wanaiomba serikali kutilia mkazo upatikanaji wa masoko ya uhakika ya
mazao ili kupanua wigo wa kibiashara kwa ajili ya kuwapatia faida
kulingana na uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Imechapishwa: 27 Januari 2016. Imeandikwa na John Nditi
Labels: FURSA NA AJIRA, KILIMO BORA, MAZAO YA VIUNGO