Kilimo cha Viungo Chachu ya Uchumi Morogoro

Milima ya Uluguru-Morogoro
ASILIMIA 90 ya wananchi katika Halmashauri ya wilaya ya Morogoro ni wakulima na wamekuwa wanakitumia kilimo kujiendeleza kiuchumi, wao na halmashauri hiyo.


Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 halmashauri hiyo inakadiriwa kuwa na watu 286,248. Kilimo cha mazao ya chakula na biashara licha ya kuwanufaisha wakulima pia ni chanzo cha makusanyo ya mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Yona Mark, anasema, ardhi katika halmashauri hiyo imegawanyika kiuzalishaji kwa mazao ya chakula, matunda na kibiashara.

Anasema kwamba halmashauri hiyo ina ukubwa wa eneo la kilometa za mraba 11,925.75 ambazo ni sawa na hekta 1,192,575 na kwamba, eneo linalofaa kwa kilimo ni hekta 447,000. Mark anataja eneo linalotumika kwa uzalishaji kwa kilimo na wakulima wadogo ni hekta 78,794.96 na jumla ya mashamba 63 yana hati miliki. Anasema eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ni hekta 28,075 , na kwamba hekta 100 zilizojengewa miundombinu ya kuvuna maji na mvua.

Hekta hizo zimetengwa kwa wakulima wa vijiji viwili, Mlilingwa na Matuli na wameanza kulima. Vijiji hivyo vyote vipo katika tarafa ya Ngerengere, kila kimoja kimepatiwa hekta 50. Anasema, ukanda wa milima unahusisha tarafa za Mkuyuni na Matombo na kwamba wananchi wa maeneo hayo wanajihusisha na uzalishaji wa kilimo cha mahindi, muhogo, migomba na magimbi. Kwa mujibu wa Mark, wananchi hao pia wanalima machungwa, mananasi, maembe, mashelisheli na mafenesi.
Mkoa wa Morogoro (Eneo lenye rangi nyekundu)
Ukanda wa mabondeni unahusisha tarafa za Mvuha, Bwakira, Mikese na Ngerengere. Wananchi kwenye maeneo hayo wanalima mahindi, mpunga, mtama, muhogo, migomba na magimbi. “Wilaya hii hutegemea kilimo kama njia kuu ya kujipatia kipato, kilimo kwa kiwango kikubwa hutegemea mvua,“ anasema Mark. Anasema, wananchi hao ni wazalishaji wa mazao mengine ya biashara likiwemo la pamba, ufuta na alizeti. Pia mazao mengine yanayozalishwa ni ya viungo ambayo ni pilipili manga, mdalasini, tangawizi, karafuu, hiliki, binzari na matunda.

Wakulima wa vijiji vya kata ya Kisemu, Tarafa ya Matombo, wanasifu uwezeshaji wa serikali kwenye kilimo. Wanasema, uwezeshaji huo ni pamoja na mafunzo ya kilimo bora, matumizi sahihi ya pembejeo hususani mbegu na dawa za kuua wadudu waharibifu wa mazao . Uwezeshaji huo pia unahusisha ujenzi wa masoko ya mazao katika baadhi ya vijiji vikiwemo vya Mkuyuni na Mtamba. Masoko hayo yamekuwa chachu ya maendeleo ya wakulima vijijini katika kuinua uchumi.

Soma Kilimo cha migomba

Mkulima katika kijiji cha Kisemu aliyejitambulisha kwa jina la Francis Kobero, anasema wananchi wa tarafa ya Matombo wanategemea kilimo cha mazao ya matunda , mboga , ndizi na mahindi kwa ajili ya kuwapatia kipato cha kila siku. “Serikali imetujengea soko la kisasa hapa Mtamba, kuwepo kwa soko hili, kumeongeza chachu ya biashara za kuuza mazao yetu kwa bei nzuri kwa wafanyabiashara kutoka nje ya wilaya” anasema Kobero.
Anasema soko limewasaidia kuuza mazao kwa bei nzuri na ziada ya faida inatumika kufanya shughuli za kimaendeleo ukiwemo ujenzi wa nyumba bora. “Mapato yanaweza kuongezeka kwa mkulima mmoja mmoja pamoja na ya halmashauri pale wakulima watakapopatiwa elimu inayohusu uzalishaji unaozingatia upatikanaji wa ongezeko lenye tija,” anasema mkulima huyo.

Soma Kilimo cha Binzari

Mkulima wa mahindi na mpunga wa kijiji cha Mtamba, tarafa ya Matombo, Agatha John anasema elimu ni tatizo kubwa kwa wakulima hivyo kusababisha washindwe kupata mafanikio endelevu ya uzalishaji mazao wenye tija. “Wakulima tukiwezeshwa kielimu ya matumizi bora ya mbegu na mbolea tutaongeza uzalisha wa chakula na ziada itauzwa kwa ajili ya kupata fedha za kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja, kijiji, kata hadi taifa,” anasema.

Anasema , mazao ya viungo, hasa pilipili manga, mdalasini , hiliki, karafuu na tangawizi yamekuwa na soko kubwa la nje ya wilaya hususani Dar es Salaam na Zanzibar. “Kila mnada wa juma unapofanyika katika masoko ya Mkuyuni, Mtamba na Mvuha , wafanyabiashara kutoka Dar es Salaam na Zanzibar wanafika kununua mazao ya viungo katika masoko haya na bei zake ni za juu,” anasema.

Soma Kilmo cha Tangawizi

Mkulima Patric Mkude , anasema katika kipindi cha nyuma wakulima walikuwa hawatumii mbolea , lakini kwa kuwa ardhi imekosa rutuba na mavuno kupatikana kidogo , wameanza kuitumia ili kuzalisha mazao kwa wingi yatakayowapatia kipato kikubwa. Wakulima wa tarafa ya Matombo, wanaiomba serikali kutilia mkazo upatikanaji wa masoko ya uhakika ya mazao ili kupanua wigo wa kibiashara kwa ajili ya kuwapatia faida kulingana na uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

SOURCE: HABARI LEO
Imechapishwa: 27 Januari 2016. Imeandikwa na John Nditi

Labels: , ,