Katika kipindi kilichopita tuliona mahitaji ya zao la vanilla na jinsi linavyolimwa, sasa leo napenda kukukaribisha ndugu yangu mkulima katika sehemu hii ya pili ambapo tutaona: magonjwa na wadudu waharibifu wa zao la vanilla likiwa shambani pamoja na kuvuna, kukausha na soko lake. Karibu...
MAGONJWA, WADUDU NA
WANYAMA WAHARIBIFU
Mmea wa vanilla kwa
kawaida haushambuliwi mara kwa mara na magonjwa au wadudu waharibifu kama
shamba limetunzwa vizuri. Mashambulizi ya magonjwa na wadudu waharibifu ni
dalili ya utunzaji duni wa shamba.
Ili kuepuka hali hiyo, ni muhimu kukagua
shamba kila wakati kubaini na kurekebisha yafuatayo:
- Nafasi kati ya mmea
na mmea ni ya kutosha kuruhusu mzunguko wa hewa safi na hivyo kupunguza hali
inayoruhusu vimelea vya magonjwa kuishi na kuzaliana.
- Kivuli kisiwe kizito
ili kuepuka giza linalowavutia wadudu waharibifu na kuruhusu vimelea vya
magonjwa.
- Kivuli chepesi
husababisha kuungua kwa majani na kufanya mmea kutokua vizuri
- Afya ya mmea ikaguliwe
kwa makini.
Kulisha marando kila
mara kunaongeza uwezo wa mizizi kuchukua chakula ardhini hivyo mmea hukua
vizuri. Mmea wenye afya nzuri haushambuliwi na magonjwa pia hustamilii
mashambulizi ya wadudu waharibifu.
Magonjwa
(i) Kuoza kwa Mizizi
(Root rot)
Ugonjwa huu
husababishwa na kuvu inayoitwa Fusarium batatis
Woollenw.var. vanillae Tucker.
Dalili
- Mmea kunyauka na
majani kuningĂinia.
- Majani kubadilika
rangi na kuanza kuwa ya manjano na hatimaye kukauka.
- Mmea kunyauka sehemu
ya chini iliyo kati ya shina na mizizi.
Kudhibiti
- Ondoa maji
yaliyotuama.
- Epuka kujeruhi
mizizi.
- Tumia dawa za ukungu
kama Bordeaux mixture 5%.
(ii) Chule ya Majani,
Matunda (Anthracnose)
Ugonjwa huu
husababishwa na aina ya kuvu inayojulikana kama Calospora vanillae Massee.
Dalili
- Mapodo na majani kuwa
na madoa ya rangi ya kahawia.
- Majani na ncha ya juu
ya shina hunyauka.
- Mizizi na mapodo na
hunyauka
- Mapodo hudondoka
Kudhibiti
- Kuzuia maji yasituame
ardhini
- Kutengeneza kivuli
chepesi,
- Kupunguza matawi
- Kuzingatia nafasi
kati ya mmea na mmea ili kuruhusu hewa safi kupita vizuri.
- Kunyunyizia dawa aina
ya Bordeaux mixture (1%) au Captafol 0.1% kabla ya mimea kuchanua.
(iii)Ubwiri Vinyoya
(Downy mildew)
Husababishwa na kuvu
aina ya Phytophthora jatrophae Jens ambao hushambulia mti wa Jatropha
unaotumika kama muega. Pia hushambulia mapodo yakiwa shambani na baada ya
kuvunwa.
Dalili: Mapodo ya vanilla na
majani ya jatropha huwa ukungu mweupe.
Kudhibiti
- Kufuata kanuni bora
za utunzaji wa shamba.
- Kutumia dawa za
ukungu kama Nitrophenol 0.518
Wadudu, Ndege na
Wanyama Waharibifu
(i) Wadudu
Wadudu wanaoweza
kushambulia vanilla ni pamoja na katapila na jongoo.
- Katapila: Hukata ncha ya mmea
inayokua
Kudhibiti: Kagua shamba mara kwa
mara ili kutambua kuwepo kwa wadudu hao na kuwaua.
- Jongoo: Hukwangua shina na
kuacha michubuko
Kudhibiti: Kagua shamba mara kwa
mara na kuwaua.
(ii) Ndege: Kuku
Huharibu mmea kwa
kuparura juu ya ardhi na kusababisha kujeruhi na kukata mizizi. Uharibifu huu
husababisha mmea kuwa katika mazingira rahisi ya kushambuliwa na vimelea kama
Fusarium batatis ambao huozesha mizizi ya mmea.
Kudhibiti: Zuia kuku wasiingie
shambani.
(iii) Konokono
Husababisha uharibifu
zaidi kipindi cha mvua. Wanapotambaa kwenye mmea huacha utando, hasa katika
sehemu inayochipua na kusababisha mmea kudumaa.
Kudhibiti
- Kagua shamba mara kwa
mara na kuwaondoa.
- Weka mchanganyiko wa
mbolea ya samadi na majivu kuzunguka shina la mmea ili kuzuia wasiweze kupanda
juu ya mimea.
UVUNAJI
Mapodo ya vanilla
hukomaa na kuwa tayari kuvunwa baada ya miezi sita hadi tisa tangu maua
kuchavushwa.
Hatua za Kukomaa kwa
Vanilla
Ukomaaji wa podo
(harage la Vanilla) la vanilla hupitia hatua tano zifuatazo:
- Podo hurefuka na
kuwa na rangi ya kijani iliyokolea.
- Ncha ya podo
hubadilika na kuwa njano.
- Rangi ya njano
husambaa taratibu katika podo.
- Ncha ya podo
hubadilika rangi na kuwa ya kahawia
- Podo hupasuka
kuanzia chini.
Jinsi ya kuvuna
Uvunaji wa zao la
vanilla huzingatia hatua za ukomaaji wa podo na njia ya ukaushaji
itakayotumika. Mapodo huvunwa kwa kukata kikonyo kutumia kisu kidogo.
- Katika hatua ya
kwanza ya ukomaaji, mapodo hayana vanillin ya kutosha hivyo yasivunwe katika
hatua hiyo.
- Mapodo yanaweza
kuvunwa yakiwa katika hatua ya pili na ya tatu endapo yatakaushwa kwa njia ya
Bourbon.
- Mapodo yanayokaushwa
kwa njia ya kukata na kukausha haraka huvunwa yakiwa katika hatua ya pili, ya
tatu na ya nne. Mapodo yasiachwe hadi kufikia hatua ya tano ya ukomaaji kwani
ubora wake hupungua.
- Uvunaji ufanyike kila
baada ya siku moja hadi mbili ili kuepuka kupasuka kwa mapodo.
- Uvunaji huendelea kwa
muda wa miezi miwili mfululizo au zaidi kulingana na ukomaaji wa mapodo.
- Marando
yaliyosisimuliwa na kutoa mapodo yakatwe na kuondolewa shambani baada ya
kuvunwa.
Mavuno
Mavuno ya zao la
vanilla hutofautina kulingana na umri wa mmea na utunzaji wa shamba. Mavuno ya
kwanza huanza kati ya miaka miwili na nusu hadi mitatu kwa wastani wa kilo moja
sawa na mapodo 50 hadi 60. Mmea unapofikia umri wa miaka minne hadi nane,
mavuno huongezeka kufikia kilo tatu hadi tano kwa mmea. Hata hivyo mavuno
huweza kupungua mmea unapofikia miaka 15 na kuendelea. Hekta moja ya shamba la
vanilla lililotunzwa vizuri hutoa mavuno tani tatu hadi tano za mapodo mabichi
sawa na wastani wa kilo 500 hadi 800 za mapodo yaliyokaushwa kwa mwaka.
Soma Kilimo cha tangawizi
UKAUSHAJI NA UHIFADHI
Mapodo ya vanilla
hukaushwa kwa njia mbalimbali kulingana na utaalamu unaotumika, vifaa vilivyopo
na matakwa ya mnunuzi. Ili kupata ubora unaotakiwa, mapodo yakaushwe mara baada
ya kuvunwa. Njia za ukaushaji zinazotumika zaidi ni Bourbon na Mexico. Njia
hizi huhitaji uangalifu na utaalamu wa kutosha ili kupata madaraja mbalimbali,
ladha, na harufu inayohitajika. Njia zote mbili hupitia katika hatua kuu nne za
ukaushaji. Hapa nchini, njia ya ukaushaji inayotumika kwa sasa ni Bourbon.
Soma kilimo cha binzari
Ukaushaji kwa Njia ya
Bourbon
Njia hii ya ukaushaji
huhusisha hatua zifuatazo:
Kuchovya Mapodo kwenye
Maji moto (Blanching).
Hatua hii huyazuia
mapodo yasiendelee kukomaa na kuanza kutoa ladha.
- Mapodo mabichi
hupangwa kulingana na ukubwa na hatua za ukomaaji.
- Mapodo hayo hupangwa
katika mafungu yasiyozidi uzito wa kilo 30 ili kurahisisha uchovyaji.
- Mapodo huwekwa na
kufungwa katika mifuko ya vitambaa maalumu vinavyoruhusu joto la maji kupenyeza
kwa urahisi.
- Mapodo yaliyovunwa
katika hatua ya pili, tatu, na nne ya ukomaaji, yatumbukizwe katika maji yenye
joto la nyuzi 60 hadi 65 za Sentigredi kwa muda wa dakika tatu hadi tatu na
nusu.
- Mapodo yaliyovunwa
katika hatua ya tano ya ukomaaji, yatumbukizwe kwenye maji ya moto kwa muda
usiozidi dakika moja.
- Mapodo yaliyochovywa
kwenye maji ya moto vizuri, huwa na rangi ya kijani iliyokolea hadi kahawia.
Kuhifadhi Joto
(sweating)
Lengo la hatua hii ni
kuongeza joto katika mapodo ili kuruhusu vimengĂenya (enzymes) kufanya kazi ya
kutoa kemikali ya vanillin ambayo huongeza ladha na harufu inayohitajika.
- Mapodo yaliyochovywa
maji moto hutolewa maji na kufungashwa katika vitambaa vyeupe na mablanketi
yanayoweza kuhifadhi joto.
- Mapodo huwekwa kwa
muda wa siku moja hadi mbili (saa 24 hadi 48) katika makasha maalumu
yanayohifadhi joto.
- Mapodo hutolewa
kwenye makasha baada ya siku moja au mbili na kutandazwa ili kuondoa yasiyo na
rangi ya kahawia.
- Katika hatua hii,
mapodo huwa na rangi ya kahawia iliyokolea.
Kukausha
Katika hatua hii,
mapodo huanikwa asubuhi au jioni wakati jua sio kali.
- Mapodo yaliyofungashwa
kwenye vitambaa vyeupe na mablanketi hutandazwa juu ya vichanja na kuanikwa kwa
muda wa saa moja au mbili.
- Baada ya saa moja au
mbili, mapodo hufungashwa tena kwenye mablanketi na kurudishwa ndani. Kazi hii
huendelea kwa muda usiopungua wiki tatu.
- Baada ya wiki tatu,
mapodo hutandazwa ndani, juu ya vichanja vinavyoruhusu hewa ya kutosha.
- Ukaushaji wa ndani
huchukua muda wa miezi mawili au mitatu.
- Ukaguzi ufanywe mara
kwa mara ili kuondoa mapodo yenye hitilafu na kutenga yaliyowahi kukauka.
Kuhifadhi Ladha
Hii ni hatua ya mwisho
katika mtiririko mzima wa ukaushaji. Katika hatua hii, mapodo huwekwa katika
makasha maalumu kwa muda wa miezi mitatu hadi mitano ili kuongeza ladha ya
vanilla.
Soma hapa fursa ya kilimo cha mazao ya viungo Morogoro
Kufungasha
Vanilla iliyokwisha
kaushwa vizuri hufungashwa kulingana na madaraja. Uzito wa kila kifungu na aina
ya ufungashaji hutegemea mahitaji ya soko.
Zao la vanilla lina thamani kubwa sana sokoni, lakini ni vizuri ufanye utafiti juu ya bei na soko lake kabla hujaanza uzalishaji. Hii itakupa uhakika na matumaini ya kukifanya kilimo hiki kwa moyo zaidi! Kama uliikosa sehemu ya kwanza isome hapa. Comment hapa chini kwa maoni au ushauri juu ya kilimo hiki.
Labels: KILIMO BORA, MAZAO YA VIUNGO, Vanila