Zao hili lilianza kuingia nchini kutoka Uganda mnamo mwaka 1954 kupitia kwa mkulima mmoja wa kijiji cha Kiilima wilaya ya Bukoba Vijijini.
UTANGULIZI
Zao la vanilla ni moja ya zao la
viungo ambalo asili yake ni Kusini Mashariki ya Mexico na sehemu nyingine za
Amerika ya Kati. Vanilla hulimwa katika nchi mbalimbali duniani. Nchi
zinazolima kwa wingi ni pamoja na Madagascar, Comoro, Tahiti, Uganda, India na
nchi nyingine za Amerika ya Kati.
Tanzania ni miongoni mwa nchi
zinazolima vanilla katika Afrika. Zao hili lilianza kuingia nchini kutoka
Uganda mnamo mwaka 1954 kupitia kwa mkulima mmoja wa kijiji cha Kiilima wilaya
ya Bukoba Vijijini. Vanilla imeanza kulimwa kibiashara hasa katika mkoa wa
Kagera mwaka wa 1992.
Katika mkoa wa Kagera, kilimo cha Vanilla kimehamasishwa
zaidi na Chama cha Maendeleo Ya Wakulima kinachofahamika kama MAYAWA. Chama
hiki kimekuwa kikihimiza uzalishaji na usindikaji wa Vanilla ambayo huuzwa
kupitia kampuni zilizopo Uganda.
Mmea wa Vanilla huzaa maharage (mapodo)
ambayo hukaushwa kwa njia maalum inayowezesha kupatikana kwa Kemikali inayoitwa
Vanillini. Kemikali hiyo hutumika katika kuongeza laadha na harufu nzuri kwenye
vyakula na vinywaji mbalimbali. Pia hutumika katika viwanda vinvyotengeneza
Vipodozi na Dawa za matibabu ya binadamu.
Kwa matumizi ya kawaida, Vanilla
huweza kutumika katika vinywaji kama Chai, Maziwa na kama kiungo kwenye mapishi ya Vyakula
mbalimbali.
Maeneo
mengine ya Tanzania yanayoweza kulima zao la vanilla ni pamoja na wilaya za
Mbeya Vijijini, Tukuyu, Morogoro Vijijini, Mvomero, Muheza, Arumeru na Ukerewe.
UMBILE LA MMEA NA
MAZINGIRA YANAYOFAA
Mmea wa Vanilla upo katika familia ya Okidi (Orchidaceae) ambayo ina
genera zipatazo 700. Kati ya hizo, genera moja itwaayo vanilla ndio yenye
umuhimu wa kiuchumi. Genera ya Vanilla ina aina au jamii zipatazo 110, kati ya
hizo ni mbili ambazo huzalishwa kibiashara. Aina hizo ni Bourbon ya nchini
Mexico na Tahitian ya visiwa vya Tahiti.
Soma: Aina mbali mbali za mbegu za mazao
Umbile la Mmea wa
Vanilla
Mmea wa Vanilla ni
rando teke linalotambaa ambalo ni la kudumu. Mmea huu hukua na kutambaa katika
mti mwingine hadi kufikia urefu wa mita 10 hadi 15 na zaidi kutegemea na
mazingira.
Mizizi
Mizizi ya mmea huu ni
mirefu ina rangi nyeupe, myembamba yenye kipenyo cha milimita mbili. Mizizi
hutokea kwenye fundo la shina lililo ndani ya udongo na hutambaa sambamba na
tabaka la udongo wenye rutuba. Pia hutokea katika vifundo vya shina sambamba na
majani ambayo hujishikiza katika miti ya kuegemea.
Shina
Shina la vanilla lina
rangi ya kijani, refu lenye vifundo na kipenyo cha sentimeta moja hadi mbili.
Nafasi kati ya fundo na fundo ni sentimita tano (5) hadi 15.
Majani
Majani yana rangi ya
kijani iliyokolea, yenye umbile la bapa, lenye ncha, nene na kubwa. Huota kwa
kupishana katika shina, yana urefu wa sentimita nane hadi 25 na upana wa
sentimita mbili hadi nane, na yana rangi ya kijani iliyokolea.
Maua
Maua yana rangi
mchanganyiko wa kijani na njano na kipenyo cha sentimita 10. Huota katika
vifungu vyenye maua kati ya 18 hadi 30.
Matunda
Matunda yana umbile la
podo la harage lenye rangi ya kijani likiwa changa. Hubadilika kuwa rangi ya
njano, hatimaye kahawia kadri linavyokomaa. Podo lina urefu wa sentmeta 10 hadi
25, kipenyo cha sentimeta nane hadi 15 na lina mbegu ndogo sana ambazo
huonekana linapokomaa.
|
Mmea wa vanilla |
Mazingira Yanayofaa
katika Uzalishaji wa Zao la Vanilla
Mmea wa vanilla una
asili ya msituni hivyo huhitaji kuoteshwa katika sehemu yenye kivuli na mvua ya
kutosha. Ili zao hili liweze kukua vizuri linahitaji mazingira yafuatayo:
Mvua
Mmea wa Vanilla
huhitaji kiasi cha mvua cha milimita 1250 hadi 2500 kwa mwaka. Pia zao hili
huhitaji kipindi cha miezi mawili cha ukame ili kuweza kusisisimka na kutoa
vitumba vya maua.
Joto
Zao hili hustawi vizuri
katika maeneo yenye nyuzi joto 20 hadi 30 za Sentigredi. Pia huweza kustahimili
nyuzi joto 32 za Sentigredi. Lakini hukua vizuri
zaidi katika kiwango cha nyuzi joto 27 za Sentigredi.
Mwinuko
Zao hili hustawi vizuri
katika maeneo yenye mwinuko wa mita 0 hadi 600 kutoka usawa wa bahari. Pia
hustawi katika maeneo yenye mwinuko unaofikia mita 1500 katika nchi za joto
(tropiki).
Udongo
Mmea wa vanilla una
mizizi ambayo hutambaa katika sehemu ya juu ya udongo. Hivyo, huhitaji udongo
mwepesi wa tifutifu, wenye rutuba ya kutosha na usiotuamisha maji.
Mwanga
Mmea wa vanilla
huathirika kwa jua na husababisha kuungua kwa majani, hivyo huhitaji kivuli cha
asilimia 50 hadi 75 ili uweze kukua vizuri. Kivuli kinaweza kupatikana kwa
kupanda miti au kwa kutengenezwa kitaalamu.
UZALISHAJI WA ZAO LA
VANILA
Vanilla huzalishwa kwa
kupandikiza marando moja kwa moja shambani au kwa kukuzwa kwanza kwenye kitalu
na baadaye kupandikizwa shambani. Kabla ya kupanda inatakiwa kuzingatia
yafuatayo:
Uchaguzi wa Shamba
Shamba la kupanda
vanilla inafaa liwe mahali pasipo na upepo mkali ili kuepuka kuanguka kwa miti
ya kuegemea na kukatika kwa mimea. Ni muhimu kupanda miti ya kuzuia upepo ikiwa
mahali hapo pana upepo mkali. Shamba hilo pia liwe na udongo usiotuamisha maji,
mwepesi na ambao unaruhusu mizizi kupenya kwa urahisi.
Aidha, shamba lisiwe na
magugu mabaya (kwa mfano kwekwe/sangare) ambayo hulazimu kutumia jembe mara kwa
mara wakati wa palizi. Kutumia jembe huweza kusababisha kukatika au kuharibu
mizizi na kuhatarisha ukuaji wa mmea.
Utayarishaji wa Shamba
Utayarishaji wa shamba
huhusisha shughuli mbalimbali kama vile usafishaji wa shamba, utayarishaji wa
mashimo na uwekaji wa mbolea.
Kusafisha Shamba
Shamba lisafishwe kwa
kulima, kungíoa visiki, magugu mabaya na kutifua hadi kina kisichopungua
sentimita 30.
Kutayarisha Mashimo
Mashimo yatayarishwe
miezi miwili hadi mitatu sambamba na usafishaji wa shamba. Yawe na kina cha
sentimita 30 na upana wa sentimita 60 hadi 90. Nafasi kati ya mstari na mstari
iwe mita mbili na nusu hadi mita tatu na kati ya shimo na shimo iwe mita moja
na nusu hadi mbili. Udongo wa juu utengwe na ule wa chini.
Uwekaji wa Mbolea
Mifumo ya Upandaji
Zao la vanilla huweza
kupandwa shambani kwa kutumia mifumo mikuu mitatu ifuatayo:
(i) Vanilla Pekee
Mfumo huu unahusisha
upandaji wa mmea wa vanilla na miti ya kuegemea tu ambayo hutoa kivuli kwa
mimea.
(ii) Vanilla na Migomba
(iii)Vanilla na Miti ya
Kivuli
Katika mfumo huu
vanilla huoteshwa katika shamba la miti ya kivuli, ambapo mmea hupandwa na miti
ya kuegemea katikati ya miti ya kivuli.
Kumbuka:
Mfumo wa pili na wa tatu unapendekezwa zaidi kutokana na matokeo yake mazuri.
Upandaji wa Miti ya
Kuegemea (miega)
Miti ya kuegemea
hupandwa miezi miwili hadi mitatu kabla ya kupanda rando la vanilla ili iweze
kuchipua, kutoa kivuli na kuwa na uwezo wa kuhimili mimea.
(i) Sifa za Miega
Miti inayofaa kutumika
kwa kuegemea iwe na sifa zifuatazo:
- Uwezo wa kukua haraka
bila kuathiri mmea wa vanilla.
- Uwezo wa kutoa kivuli
kinachofaa.
- Uwezo wa kuchipua
haraka inapopunguzwa.
- Uwezo wa kuchipua
matawi kwa chini ili kupandishia marando kwa urahisi.
- Uwezekano wa
kuoteshwa kwa urahisi.
Miti yenye sifa hizo ni
pamoja na mibono (Jatropha carcus) na Gilirisidia. Miti mingine inayoweza
kutumika kwa kivuli na kuegemea ni pamoja na Erythrina spp na Bauhania spp.
(ii) Kupanda Miega ya
Mibono
Miti inayotumika zaidi
katika mashamba ya vanilla ni jamii ya Jatropha. Miti hii huoteshwa kwa kutumia
mbegu au kipande cha tawi kwa umbali wa sentimita 30 kutoka katika shimo la
kupandia vanilla. Tawi la mbono lenye
urefu wa sentimita 120 hadi 150 hupandwa katika kina cha sentimita10 hadi 15.
Upandaji wa Vanilla
Mmea wa vanilla
hupandwa mwanzoni mwa msimu wa mvua ili kuhakikisha upatikanaji wa unyevu
ardhini. Hupandwa kwa kutumia rando lenye urefu wa kati ya sentimita 100 hadi
150 (futi tatu na nusu hadi tano) kutoka kwenye mmea unaokuwa vizuri, usio na
magonjwa na wenye pingili ndefu. Rando lenye sifa hizo hukua haraka na kutoa
maua mapema (miaka 2). Rando fupi halikui haraka na huchukua muda mrefu kutoa
maua (miaka 2 hadi 3).
Kutayarisha Marando
- Kata rando kwa
kutumia kisu kikali kwa kufuata vipimo (sentimita 100 hadi 150).
- Ondoa majani matatu
hadi matano katika sehemu ya chini ya rando itayofukiwa kwenye udongo.
- Ning'iniza rando
lililokatwa kwenye kivuli kwa muda wa siku saba hadi 10 kabla ya kupanda ili
kupunguza utomvu na kulipa nguvu ya kuchipua na kuhimili hali ya shambani.
Jinsi ya Kupanda
Upandaji wa vanilla
hufanywa kwa kutumia hatua zifuatazo:
- Andaa nyasi kavu
(matandazo) ambazo zitatumika mara baada ya kupanda.
- Tengeneza kifereji
chenye kina cha sentimita 10 hadi 12 katikati ya shimo lenye mbolea
lililokwisha tengenezwa.
- Laza sehemu ya rando
iliyotolewa majani katika kifereji hicho, acha sehemu yenye majani juu ya
ardhi.
- Fukia rando kwenye
kifereji kwa udongo na gandamiza taratibu ili lishikamane na udongo.
- Funga sehemu ya juu
ya rando kwa kutumia kamba katika umbile la nane kwenye mti wa kuegemea.
- Weka matandazo
kuzunguka kila shina lililopandwa.
Kumbuka:
- Utaratibu huu wa
kupanda hutumika katika aina zote za mifumo ya kuzalisha vanilla, na
hutofautiana kwa nafasi za upandaji kati ya mfumo mmoja na mwingine.
- Shamba la vanilla
pekee katika miaka ya mwanzoni, huweza kuchanganywa katikati ya mistari na
mazao mengine ya muda mfupi kama mazao ya jamii ya mikunde.
Utunzaji wa Shamba
Vanilla huhitaji
kutunzwa vizuri ili iweze kukua vizuri na kutoa mavuno yenye ubora wa hali ya
juu. Huduma muhimu katika uzalishaji wa vanilla ni kama ifuatavyo:
Kutengeneza Kivuli
Mmea wa vanilla huhitaji
kivuli ili uweze kukua vizuri. Hivyo ni muhimu kupanda miti ya kivuli kabla ya
kustawisha vanilla. Katika ukuaji wake
kuanzia inapopandwa hadi inapokaribia kutoa maua huhitaji kivuli cha kutosha
kinachoweza kuzuia jua kali na kuruhusu mwanga (asilimia 60 hadi 70).
Kipindi
cha kusisimua kivuli kipunguzwe zaidi na kufikia asilimia 55 hadi 50. Kivuli kitengenezwe kwa
kupunguza matawi ya miti ya miega na ya kivuli ili kupata kivuli kinachofaa.
Kumbuka: Kivuli kizito huathiri
ukuaji wa mmea.
Kuweka Matandazo
Utandazaji wa nyasi ni
muhimu katika shamba la vanila kutokana na tabia ya ukuaji wa mizizi ambayo
huota katika kina cha sentimita 5 hadi 10, hivyo huhitaji kulindwa isiharibiwe. Matandazo yawekwe
kuzunguka mashina ya mimea ili kuhifadhi unyevu, kuzuia uotaji wa magugu, na
kulinda mizizi isiharibiwe wakati wa palizi.
Kumbuka: Matandazo yawe makavu
na yasiwe na mbegu za magugu.
Palizi
Palizi hufanyika wakati
wowote magugu yanapoota shambani. Inashauriwa kufanya palizi kabla ya mvua
kunyesha ili mmea uweze kutumia maji ya mvua ipasavyo. Palizi ifanyike wakati
wowote magugu yanapoota shambani, kwa kungíoa magugu kutumia mikono ili kuepuka
kujeruhi mizizi jembe linapotumika.
Kuning’iniza Marando
Mmea wa vanilla uliokua
vizuri huota matawi (marando) mengi na marefu. Marando hayo huelekezwa kwenye
matawi ya miti ya kuegemea na kuningíinizwa. Rando linapofikia urefu
wa sentimita 150 hadi 180 liningíinizwe katika matawi ya miega ili liendelee
kukua kuelekea chini. Endapo kuna upepo mkali, marando yafungwe kwenye miega
kwa muda ili yasivunjike.
Kulisha Marando
Kulisha marando ni
kitendo cha kufukia ardhini sehemu ya kipande cha rando ili kiweze kutoa mizizi
na kuongeza nguvu ya kuchukua chakula kutoka kwenye udongo. Kazi hii hufanywa
baada ya rando lililoningíinizwa kurefuka sana kiasi cha kutambaa ardhini,
katika hatua hii mmea huweza kuwa na umri wa miezi sita hadi tisa kutegemea na
utunzaji.
Jinsi ya Kulisha
- Ondoa majani matatu
hadi manne kwenye rando lililoingíinizwa na kurefuka sana.
- Fukia kwenye udongo,
karibu na shina sehemu iliyoondolewa majani.
- Weka matandazo katika
sehemu iliyofukiwa ili kuhifadhi unyevu.
- Funga sehemu ya juu
ya rando katika mti wa kuegemea ili liendelee kukua.
- Marando mawili hadi
mitatu yalishwe kwa wakati mmoja na mengine yaachwe kwa ajili ya kutoa maua na
kupata marando ya kupanda.
Kumbuka: Kulisha
kufanyike wakati wa mvua ili marando yaweze kutoa mizizi kwa urahisi. Kazi hii
irudiwe kila wakati ili rando mama litakapokatika machipukizi yake yaendelea kukua.
Soma kilimo cha tangawizi
Kusisimua
Kusisimua ni kitendo
cha kuufanya mmea kuwa katika hali ya kuweza kutoa maua. Kitendo hiki kifanywe
wakati mmea ukiwa umefikia umri wa mwaka 1 na nusu au zaidi, na hufanywa wakati
wa kiangazi ili kuepuka kupata matawi mengi badala ya vitumba vya maua. Mmea
usiosisimuliwa hautoi maua au hutoa maua machache na kusisimua mapema kunaweza
kuuchosha mmea.
Jinsi ya Kusisimua
- Chagua matawi matatu
hadi matano yanayoningíinia. Kusisimua matawi mengi kunaweza kuudhoofisha mmea
au kuzaa maharage madogo.
- Kata ncha ya rando
ili kuwezesha vitumba vya maua kukua na kuwa tayari kufunguka au kutoa maua.
Ukataji wa ncha huweza
kufanyika kama ifuatavyo:
- Kukata ncha ndogo
(mdomo wa rando) kwa mkono. Hii hufanyika kwa rando fupi linaloningínia.
- Kukata rando kwa kisu
kikali, kwa rando linaloningínia ambalo halijafikia urefu wa kupanda.
- Kukata rando kwa kisu
kikali kwa rando refu linaloningíinia (lenye urefu wa kuweza kupandwa,
sentimita100-150).
Uchavushaji
Ni kitendo cha
kuunganisha chavua kutoka katika sehemu dume ya ua na kuweka katika sehemu jike
ya ua, hufanyika baada ya maua kuchanua.
Uchanuaji wa Maua
Mmea wa Vanilla hutoa
maua miezi miwili hadi mitatu baada ya kusisimuliwa. Maua huchanua kwa kipindi
cha masaa matatu hadi manne kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa saba mchana kwa
muda wa miezi miwili hadi mitatu kutegemea unyevu uliopo kwenye udongo na
kiwango cha Jua.
Ua huchanua kwa muda huo na hudondoka baada ya siku 1 ikiwa
halikupata chavua. Hivyo ni muhimu uchavushaji ufanyike kwa haraka na kwa
uangalifu mkubwa.
|
Maua ya vanilla |
Jinsi ya Kuchavusha
Mmea wa vanilla, ili
uweze kutoa matunda inabidi uchavushwe. Ua la vanilla kwa kawaida huchavushwa
na nyuki jamii ya melapona ambao hawapo hapa nchini. Nyuki hao hupatikana
Mexico na katika nchi nyingine za Amerika ya Kati. Hivyo uchavushaji hufanywa
kwa mikono kwani umbile la ua haliruhusu nyuki wa aina nyingine kufanya
uchavushaji.
Soma kilimo cha binzari
Uchavushaji hufanywa
kwa kufuata hatua zifuatazo:
- Gawa petali ya ua la
vanilla katika sehemu mbili kwa kutumia pini, sindano, au mwiba. Hakikisha
vifaa hivyo ni safi.
- Kunjua sehemu jike ya
ua (stigima) kwa kuelekea juu ili kuwezesha kulala sambamba kwenye sehemu dume
ya ua (stameni).
- Unganisha stameni na
stigima na kubana taratibu kwa dole gumba kwa nusu dakika ili kuruhusu chavua
kuingia kwenye stigima.
Ua lililochavushwa
vizuri, hubaki likiningíinia kwenye kikonyo chake. Ikiwa uchavushaji
haukufanikiwa, ua hudondoka baada ya siku moja au mbili. Kiasi cha maua au
mapodo nane hadi 12 yaachwe katika kila kitumba. Aidha vitumba vinne hadi nane
viruhusiwe kukua katika kila rando na visizidi 20 kwa mmea.
Ndugu yangu mkulima hivi ndivyo vanilla inavyolimwa, ni shughuri nzito sana lakini inalipa sana, kama ilivyo kawaida: mvumilivu hula mbivu. Sasa badilishana nasi uzoefu wako wa kilimo hiki kwa ku-coment hapa chini huku ukisubiri muendelezo wa kilimo cha vanilla.
Labels: KILIMO BORA, MAZAO YA VIUNGO, Vanila