Utangulizi
Karanga
ni mojawapo ya mazao yanayotoa mafuta. Katika Tanzania zao hili hustawi zaid
katika mikoa ya Kusini Mashariki, Dodoma na Morogoro. Pamoja na kutoa mafuta
vile vile zao hutumika kwa njia nyingine mbali mbali, nazo ni pamoja na:
Chakula cha wanyama / mifugo (Mashudu na majani), kurutubisha ardhi na chakula
cha binadamu: kutafuna na kuunga kwenye mboga/chakula (Confectionary)
Kwa
ujumla zao hili hutumika na wakulima kama zao la biashara.
Hali
ya Hewa
Karanga
hustawi vizuri katika maeneo yaliyopo kwenye miinuko chini ya mita 1500 toka
usawa wa bahari katika Tanzania, na hustawi zaidi katika maeneo ambayo yanapata
mvua za wastani wa mm 750 hadi mm 1200 kwa mwaka.
Vile
vile karanga hustawi vizuri kwenye udongo wa kichanga, inashauriwa kutopanda
karanga kwenye udongo mzito (mfinyanzi) hii ni kutokana na sababu kwamba,
karanga hazistawi kwenye sehemu zinazo simama maji, na udongo mzito huleta
hasara wakati wa uvunaji.
Mbegu Bora Za Karanga
Kuna
mbegu nyingi za karanga lakini zilizotangazwa hivi karibuni na zinazofanya
vizuri zaidi ni hizi zifuatazo:
Utayarishaji
Wa Shamba
Shamba
litayarishwe vizuri kuwezesha udongo kupenyesha maji na mizizi kirahisi.
Karanga hupandwa kwenye matuta au sensa.
Utayarishaji
Wa Mbegu
Karanga
ambazo zinakusudiwa kwa mbegu zitunzwe na maganda yake bila kubanguliwa.
Zibanguliwe karibu na msimu wa kupanda na kuchaguliwa. Baada ya kuchaguliwa
zitiwe dawa, aina ya Fernasan D, Katika uwiano wa gramu
28 za dawa kwa kila kilo 10 za mbegu safi.
Upandaji
Wa Karanga
Wakati
wa kupanda: Uamuzi
wa kuchagua wakati mzuri wa kupanda ni ule utakaoliwezesha zao hilo kukomaa
wakati wa mvua za mwisho. Kuchelewa kupanda, hupunguza mavuno. Ni muhimu
kuchagua aina ya mbegu ambazo uvunaji wake unafanana na mazingiza ya eneo hilo
kihali ya hewa.
Kwa mikoa ya Kusini: karanga za muda wa kati na mrefu
(Johari, Red Mwitunde) zipandwe kuanzia katikati, hadi mwishoni mwa mwezi
Desemba. Karanga za muda mfupi (Spanish na Valencia) zipandwe kuanzia mwishoni
mwa mwezi Desemba hadi katikati ya mwezi Januari.
Kwa mikoa ya mashariki na sehemu za mkoa wa
Dodoma: karanga zipandwe mapema mwanzoni mwa
mvua ndefu (Februari / March).
Nafasi
Kati Ya Mimea
Inashauriwa
kupanda karanga katika mistari. Nafasi kati ya mistari ni sentimita 50, na kati
ya mimea ni sentimita 15 kwa karanga zinazotambaa (Virginia Spreading types).
Kama karanga zinapandwa kwenye matuta ya sentimita 90, zipandwe mistari miwili,
kila tuta. Kwa nafasi hii kiasi cha kil 60-75 za mbegu hutumika kwa hekta moja.
Kwa
karanga zilizopo kwenye kundi la Spanish/Valencia (zisizotambaa), nafasi kati
ya mistari ni sentimita 50, na kati ya mimea ni sentimita 10. Endapo karanga
zimepandwa kwenye matuta ya sentimita 90, panda mistari miwili, inayofanya
nafasi sawa na sentimita 50 kwa sentimita 10. Kiasi cha kilo 80-100 za mbegu
hutumika kwa hekta moja kwa kutumia nafasi hii. Ambapo ni sawa sawa na kilo 32
hadi 40 kwa ekari.
Kwa aina
zote za mbegu, panda mbegu moja safi, katika kila shimo.
Mahitaji
Ya Mbolea Ya Karanga
Kufuatana
na majaribio yaliyofanyika imeonekana kuwa karanga hustawi vizuri chini ya
viwango vidogo vya phosphorus. Vyanza vya kirutubisho cha Phosphorus ni mbolea
za kupandia nazo ni kama TSP, SSP na DAP. Mbolea hizi zote ziwekwe kabla ya
kupanda au wakati wa kupanda lakini umakini unahitajika kutoruhusu mbolea
kugusana na mbegu. Kiasi cha Kilo 90 za Phosphorus (= mifuko minne ya DAP)
kinatosha kwa hekta moja ambayo ni sawa sawa na kilo 35 (= mfuko mmoja na nusu
wa DAP) kwa ekari.
Vile
vile katika sehemu nyingine, karanga zimefanya vizuri kwa kutumia samadi.
Ubadilishaji wa mazao (Crop Rotation) husaidia kutunza rutuba, hivyo kupunguza
kiasi cha mbolea kinachotumika. Karanga zinaweza kulimwa baada ya mahindi, ili
kutumia masalia ya mbolea.
Upaliliaji
Karanga
zipaliliwe zikiwa changa. Shamba lililotayarishwa vizuri na kuondolewa magugu
ya muda mrefu (Perrenial weeds) linaweza kupalliwa mara moja, kwa sababu
karanga hukua haraka, na zinaweza kushindana na magugu. Baada ya kutoa maua,
karanga zisipaliliwe, hii inaweza kuharibu 'pegs', hatimaye kupunguza mavuno.
Magonjwa
Na Wadudu Waharibifu Wa Karanga
Magonjwa
Hatari Ya Karanga
(i) Ugonjwa wa kuoza (Aflatoxin)
Katika
hali ya unyevu mwingi vimelea viitwavyo Aspegilus flavus huota ndani ya
maganda na kushambulia mbegu za karanga. Vimelea hivyo hutoa kemikali ambayo ni
sumu.
Kuzuia
- Hakikisha kuwa karanga haziharibiwi
wakati wa kuchimba.
- Hakikisha karanga zinakaushwa vizuri
(Unyevu wa 10%) kabla ya kuzitunza zitumike kama mbegu
- Karanga za kupanda zitiwe dawa aina ya
Fernasan-D.
Magonjwa
haya husababisha madoa ya rangi ya kikahawia hadi meusi kwenye majani. Vimelea
vinavyosababisha magonjwa haya viko vya aina tatu:
- Cersospora
arachidicola. Husababisha Early Leaf Spot.
- Phaeoisariopsis
personata. Husababisha Late Leaf spot. Ugonjwa
wa Early Leaf Spot hutangulia kuonekana, lakini magonjwa yote mawili yanaweza
kujitokeza shambani kuanzaia wiki 3-5 baada ya karanga kupandwa.
- Puccinia arachidis. Husababisha ugonjwa wa Kutu.
Kuzuia
- Kupanda mapema.
- Kuondoa maotea ya karanga wakati wa
kiangazi.
- Tumia dawa aina ya Chlorothalonil
(Daconil 2787)
Dawa
huwekwa kiasi cha kilo 1.6 katika lita 800 za maji kwa hekta moja, kila baada
ya siku saba, kwa majuma machache kuanzaia maratu dalili za ugonjwa
zinapoonekana. Uchunguzi
juu ya aina zinazostahimili magonjwa haya bado unaendele kufanywa Naliendele.
Soma hapa magonjwa ya vitunguu maji na madawa yake
(iii) Ugonjwa wa Rosette (Rosette virus disease)
Ugonjwa
huu huambukizwa na wadud waitwao "Vidudu Mafuta" Aphids (Aphis
cracivora). Mimea ambayo imeshambuliwa na ugonjwa huu hudumaa, na inakuwa na
madoa ya njano.
Kuzuia
- Kupanda mapema
- Panda karanga zako shambani katika
nafasi za karibu karibu.
- Palilia na toa maotea shambani mwako.
(iv) Ugonjwa wa
maganda matupu (Empty pods or pops)
Karanga
zilizoshambaliwa na ugonjwa huu, huwa lazina mbegu (maganda matupu). Ugonjwa
huu husababishwa na ukosefu wa madini ya Calcium (chokaa) kwenye udongo.
Kuzuia
Tumia Calcium katika hali ya Gypsum
(Ca SO4) kwenye mimea au weka Chokaa (lime - CaO) kwenye udongo kabla ya
kupanda. Ugonjwa huu uko kwenye mikoa ya kusini mwa Tanzania (Lindi, Mtwara na
Ruvuma) na hushambulia sana karanga za muda mrefu kama vile Red Mwitunde.
Majaribio
hapa Tanzania hayajathibitisha kuweka chokaa (Liming) kuwa ni jibu sahihi la
kupambana na ugonjwahuu, lakini ili kupunguza, kupanda mapema ni muhimu.
Wadudu
Waharibifu Wa Karanga
(i)
Mafuta Aphids au "Vidudu Mafuta" (Aphis cracivora)
Hushambulia
karanga kila msimu, lakini athari yao kubwa ni kueneza ugonjwa wa Rosette.
Wakati wa mvua nyingi huoshwa toka kwenye majani, hivyo hawaleti madhara.
Kuzuia
- Kupanda mapema
- kupanda karanga karibu karibu
(ii)
Groundnut hopper: Hilda patruelis
Hufyonza mizizi, "pegs", na karanga changa, hivyo
husababisha majani kuwa manjano, kunyauka, na mmea kukauka ungali mchanga.
Wadudu hawa hushambulia mazao mengine kama vile maharage, kunde. alizeti na
korosho, hivyo kunahitajika mzunguko (rotation) mzuri wa mazao.
Kuzuia
- Kwenye mashamba makubwa, inashauriwa
kutumia dawa aina ya Aldrin au chloropyrifos,
kuchanganya kwenye ardhi kabla ya kupanda.
- Kunyunyizia Dimethoate mara tu wadudu
wanapoonekana
- Kutochanganya na zao la korosho au
mbaazi kwenye shamba moja na karanga.
(iii)
Mchwa
Kuna
aina mbili za mchwa ambao hushambulia na kusababisha uharibifu kwenye zao la
karanga.
Aina ya kwanza ni wale ambao hutoboa sehemu ya chini kwenye
mzizi, au kutengeneza matundu, na hukaa kwenye mmea wa karanga wakati wote
zikiwa shambani.
Aina ya pili ni wale ambao hukata matawi yanayokua
au kutambaa. Uharibifu huu huonekana zaidi kwenye shamba jipya. Kuchelewa
kuvuna kunaweza kusababisha kupotea kwa mazao mengi, kutokana na kuharibika kwa
mizizi, na kusababisha karanga nyingi kubakia shambani wakati wa kuvuna.
Kuzuia
Mchwa
wanaweza kuzuiwa kwa kutumia dawa aina ya Alandrin 40% ya unga, kwa kiasi cha
kilo 2.5 kwa hekta. Njia rahisi ni kuchanganya dawa na mbolea aina ya Phosphate
(TSP au SSP) au mchanga na kumwaga shambani kabla ya kupanda karanga.
(iv)
Panya
Hushambulia
sana karanga zinapoanza kuota, na wakati zinapokaribia kuvunwa.
Namna ya Kuzuia panya:
- Tumia dawa za kuua panya
- Mitego
- Kuwachimbua toka ardhini
walikojificha.
(v)
Ndege
Kama
panya, ndege hasa kunguru hushambulia sana karanga kabla hazijaota (mara baada
ya kupanda), zinapoanza kuota, zinapokaribia na wakati zimekwisha komaa.
Kuzuia
Kung’oa Karanga
Utajuaje kama karanga
zako zimekomaa? Zifuatazo ni baadhi ya dalili za jumla ambazo huonekana kwenye
karanga zilizokomaa:
- Angalia majani: huwa yanabadilika rangi kuwa ya manjano na kuanza
kupata au kuongezeka ugonjwa wa madoa madoa na hatimaye kudondoka
- Ukichimba na kuangalia mapodo yanaonekana kuwa magumu na hupasuka kwa
urahisi. Podo la karanga ambazo hazijakomaa huwa laini na hubonyea
linapominywa.
- Rangi ya ndani ya podo hubadilika kutoka nyeupe na kuwa ya kahawia.
- Ukichimba karanga (katika maeneo mbalimbali ya shamba) na ukapata
mashina saba au zaidi yaliyokomaa katika kila mashina 10, basi karanga zako
zimekomaa, ngo’a.
- Zinapokaribia siku za kukomaa kutokana na idadi ya siku inazochukua
tangu kupanda hadi kukomaa. Hakikisha unakumbuka aina ya mbegu uliyopanda na muda
inayotumia kukomaa, zichunguze karanga kadri zinavyozidi kukaribia.
|
Karanga zilizong'olewa |
Kupurura Karanga
Kupurura ni kutenganisha
mapodo ya karanga na shina. Tenganisha mapodo ya karanga na shina kwa kutumia
mikono. Mapodo ya karanga pia yanaweza kupururwa kwa kutumia ncha ya jembe au
pipa lililokatwa. Ukishapurura unapata karanga za mapodo. Shughuli hii
hufanyika mara tu baada ya kung’oa. Mara baada ya kupurura, karanga za mapodo
huchambuliwa na baadae kuanikwa juani ili zikauke na kuhifadhiwa mpaka zitakapo
hitajika kwa matumizi au kuuza.
Kuchambua Karanga
Chambua mapodo ya karanga
zilizopururwa kwa kutenga yaliyosinyaa, yasiyo na punje, yaliyooza au
kutobolewa na wadudu. Lengo la kuchambua ni kupata mapodo ya karanga yaliyo
bora. Mapodo ya karanga bora yatengwe tayari kwa kukaushwa au kusafirishwa.
|
Kuchambua karanga |
Kukausha Karanga
Mapodo ya karanga
hukaushwa vizuri ili kudhibiti uwezekano wa karanga kushambuliwa na magonjwa
yatokanayo na ukungu wakati wa kuhifadhi. Kausha juani kwa kutandaza mapodo
kwenye kichanja bora, maturubai au sakafu safi. Wakati wa kukausha zingatia
yafuatayo:-
- Hakikisha punje za karanga zimekauka hadi kufikia unyevu wa asilimia 9
kwa kutumia kipima unyevu au kadiria tu utakapoona zimekauka kiasi cha kutosha.
- Ukaushaji wa kupita kiasi husababisha ngozi ya punje ya karanga kutoka
wakati wa kubangua na hivyo kupunguza ubora wa zao.
- Baada ya kukausha, fungasha mapodo ya karanga safi kwenye magunia
yasiyozidi kilo 75.
Kuhifadhi
Karanga Za Mapodo
Ili kuepuka uharibifu ni
muhimu kuhifadhi karanga zikiwa kwenye mapodo. Karanga zilizobanguliwa
huhifadhiwa kwa muda mfupi na hushambuliwa kwa urahisi na nondo na kusababisha
upotevu kwa kiasi kikubwa. Hifadhi ya karanga zikiwa kwenye mapodo huwezesha
karanga kuhifadhiwa kwa zaidi ya mwaka mmoja wakati zile zilizobanguliwa huweza
kuhifadhiwa kwa muda usiozidi miezi miwili.
Kabla ya kuweka karanga
ghalani zingatia yafuatayo: -
- Safisha ghala ili
kuondoa wadudu waharibifu na takataka.
- Ziba sehemu zote ambazo
zinaweza kuruhusu panya na wadudu wengine kuingia.
- Magunia yapangwe kwa
kupishanisha ili kuruhusu mzunguko wa hewa.
- Karanga pia zinaweza
kuhifadhiwa zikiwa katika hali ya kichele kwenye bini, silo, au vihenge.
Kubangua Mapodo Ya Karanga
Mapodo ya karanga
hubanguliwa kwa kutumia mikono au mashine.
Kubangua kwa kutumia mikono
Mapodo
ya karanga hubanguliwa kwa kuminya ganda kwa kutumia vidole. Njia hii ni ya suluba, huchukua muda mrefu na
hufaa kwa kiasi kidogo cha karanga. Hata hivyo njia
hii hupungu za upotevu wa mazao. Vilevile punje za karanga huwa bora
Zaidi zinapobanguliwa kwa njia hii.
Kubangua karanga ni kazi ngumu sana. Mtu mmoja anaweza kubangua
kiasi cha kilo 12-15 kwa siku. Karanga zilizopo kwenye kundi la Virginia
hubangulika kirahisi kuliko aina ya Spanish au Valencia. Mashine za
kubangulia karanga hupatikana hapa nchini, zinarahisisha kazi, lakini tahadhari
isipochukuliwa huharibu karanga. Wastani wa kilo 160 za karanga zilizo
kwenye mapodo hutoa kilo 100 za punje za karanga na kazi hii huchukua siku nane
kwa mtu mmoja.
Kubangua kwa mashine
Mapodo ya karanga hubanguliwa
kwa kutumia vyombo maalumu. Njia hii hubangua karanga nyingi zaidi na kwa muda
mfupi. Mashine hizi huendeshwa kwa mkono, umeme au injini. Hurahisisha kazi na
zina uwezo wa kubangua wastani wa kilo 40 kwa saa moja.
Kuchambua Karanga Zilizobanguliwa
- Punje za karanga zilizosinyaa, zenye ukungu, zilizopasuka,
zilizoharibiwa na wadudu na zilizokatika zitenganishwe na karanga bora.
- Punje za karanga zilizooza na zenye magonjwa zisitumike kwa chakula cha
binadamu wala wanyama.
- Chambua kwa makini karanga zilizobanguliwa kwa kutumia vyombo maalum
kwani nyingi hupasuka kutegemea aina ya karanga, ukavu wa mapodo na ufanisi wa
mashine.
Kupanga Madaraja
Madaraja ya punje za
karanga hupangwa kufuata ukubwa, aina na rangi. Pia zingatia viwango vya ubora
vilivyowekwa kwa kila daraja la punje za karanga. Punje za karanga zilizo
katika daraja la chini zitumike haraka kwani hushambuliwa na vimelea vya ukungu
kwa urahisi zaidi. Punje za karanga zilizo bora (daraja la 1) zitumike kwa
kuhifadhi, kuuzwa au kusindikwa.
Kufungasha
Fungasha karanga
zilizobanguliwa kwenye magunia yenye ujazo usiozidi kilo 100. Karanga
zilizobanguliwa zisihifadhiwe kwa muda mrefu, kwani hushambuliwa kwa urahisi na
wadudu aina ya nondo na vimelea vya magonjwa ya ukungu.
Usiache kusoma...
Labels: KILIMO BORA